Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
imeanza kufanya tathmini na mchakato wa mapitio ya Sera ya Maendeleo na Huduma
kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Akifungua kikao cha wadau jana jijini Dodoma cha kupitia
taarifa ya awali ya mapitio hayo, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Jamal
Katundu, amesema mapitio hayo yanafanywa na serikali kwa kushirikiana na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN
WOMEN) huku akitaka yazingatie uwakilishi wa makundi yote ya Watu wenye Ulemavu
ili kuwa na sera bora.
Naye, Mwakilishi wa UN WOMEN, Jacob Kayombo, amesema shirika
limeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya mchakato huo na kwamba wanaamini
itakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Watu
Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Jonas Lubago, ameishukuru serikali kwa kutimiza
ahadi ya kufanya maboresho ya sera hiyo na kuahidi kushiriki kikamilifu ili
kuwa na maboresho mazuri ya sera.
Awali, Mshauri Elekezi ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Consolata Sulley, amesema katika hatua ya awali
ya mapitio utafanyika utafiti kwa kupata maoni kutoka kwa wadau ili kuwa na
sera bora inayozingatia haki na masuala ya kijinsia kwa Watu wenye Ulemavu.
Na. Mwandishi Wetu- Dodoma
0 Maoni