WAZIRI MKUU Mh. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo
iweke katika lugha rahisi andiko juu ya upatikanaji wa mitaji na pembejeo kwa
wakulima na wafugaji.
“Niendelee kuzitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi ziandae utaratibu wa kuziweka kwenye mifumo rahisi na kuzifikisha kwa
wakulima na wavuvi maelezo juu ya upatikanaji wa mitaji, kupata pembejeo kwa
urahisi na kuifikia teknolojia mpya.”
Ametoa agizo hilo leo Agosti 3,2023 baada ya kukagua mabanda
ya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini
Mbeya.
Akizungumza na wadau na washiriki wa maonesho hayo, Waziri
Mkuu amesema akiwa ziarani Urusi, wiki iliyopita alikutana na mwekezaji wa
mbolea ambaye anataka kuja kuwekeza nchini. “Bado mahitaji ya mbolea ni
makubwa, bado tuna mahitaji ya masoko na teknolojia kwa wavuvi na wakulima.
Elimu iendelee kusambazwa juu ya upatikanaji wa mbolea,” amesisitiza.
Akielezea kuhusu maonesho hayo, Waziri Mkuu amesema maonesho
ya mwaka huu ni mazuri zaidi ya mwaka jana kwani ameona kuna teknolojia nyingi
mpya ambazo zimebuniwa na vijana.
“Kama tutaendelea kulima na kufuga hivi, tunaweza kusema
sasa sekta ya kilimo imeanza kwenda kwenye mwelekeo mzuri. Tanzania iko vizuri
kijiografia na imekaa kimkakati, kwa hiyo tukiwa na uzalishaji mzuri wa chakula
na mazao ya kibiashara, tukafuga kibiashara na kuvua kibiashara tutaweza
kulisha nchi jirani na wakulima wenyewe wataweza kunufaika.”
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliongeza bajeti za
wizara hizi mbili na ya kilimo kwa mfano imefikia bilioni 900. Niwasihi
Watanzania wenzangu, tuingie kwenye biashara ya ufugaji. Leo tumeona namna ya
kufuga na kunenepesha mifugo. Hili ndilo eneo tunatakiwa tulikimbilie kwani
litaleta manufaa ya mtu mmoja mmoja.”
Amewataka wakazi wa Mbeya na mikoa ya jirani watumie
maonesho hayo yanayoendelea kufanyika hadi Agosti 8, mwaka huu, ili kujifunza
teknolojia mbalimbali mpya.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan juu
ya mpango wa kuwawezesha vijana kulima kibiashara (BBT), Waziri Mkuu amesema
yafanyiwe kazi na hasa suala la kufanya kazi kwenye eneo kijana alitakalo.
“Vijana waliojiunga na mpango wa BBT, walioanza mafuzo mwaka
huu, wamekaribia kuhitimu. Eneo la BBT liko pia kwenye mifugo. Unaweza kupewa
eneo, ukaweka mifugo na kuwanenepesha. Kubwa zaidi ni upatikanaji wa mitaji,”
amesema.
Kuhusu mabenki kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi,
Waziri Mkuu aliwataka waangalie uwezekano wa kushusha riba zaidi. “Nimepitia
mabanda ya mabenki na kuwauliza kuhusu riba. Wengi wao wameshusha kutoka
asilimia 12 au 13 ya awali na wamefika asilimia tisa. Naamini wataendelea
kushusha zaidi,” amesema Waziri Mkuu ambaye alikagua mabanda ya benki za
Azania, CRDB, STANBIC, NBC na TADB.
Kuhusu ushirika, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo,
Hussein Bashe asimamie usajili, mapato, matumizi na mwenendo wa AMCOS ili
ziweze kuleta tija kwa wakulima.
“Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri upo hapa, hakikisha AMCOS ambazo
hazijasajiliwa zijulikane, na kama kweli wanataka kuanzisha AMCOS warasimishwe,
lakini kama zipo ambazo hazieleweki waandalieni utaratibu ili waweze kujiunga
na AMCOS ambazo zipo rasmi.”
Waziri Mkuu amesema kuwa ushirika ni mfumo mzuri ambao
unaweza kuwafikia wananchi kwa namna mbalimbali ikiwemo elimu, masoko au
kuwapelekea pembejeo. “Ushirika unatusaidia pia kupata sauti ya wakulima kuja
serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi, ndiyo maana tunataka ushirika huu
usajiliwe”
Mapema, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema
wana banda kubwa kwenye maonesho hayo ambalo wanatumia vijana kuonesha
teknolojia ya kunenepesha mifugo ili kusaidia kubadilisha mtazamo wa wafugaji
nchini.
“Wizara yetu tumedhamiria kuwatumia vijana, kwa hiyo
tutaingia mkataba wa makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa ili asilimia 40 ya
vijana watoke jeshini, asilimia 30 iwe ni wataalamu wetu na asilimia 30
iliyobakia iwe ni vijana kutoka maeneo mengine ya asili,” alisema.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa
maonesho hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hai ya uzalishaji
chakula hapa nchini nzuri kwani mikoa ya uzalishaji imeongezeka kutoka mitano
ya awali hadi 13.
“Sasa hivi hatuzungumzii Big 5 au Big 6 bali tuna mikoa 13
ya uzalishaji wa chakula nchini. Mikoa hiyo, mwaka huu imezalisha zaidi ya
asilimia 70 ya chakula chote nchini,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 03, 2023.
0 Maoni