WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ihakikishe kuwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanatengwa na yanatumika katika sekta husika kulingana na miongozo iliyopo ili kuboresha sekta hizo.
“Ofisi ya Rais (TAMISEMI) hakikisheni mnasimamia Mwongozo wa
Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 unaozitaka
Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mapato ya ndani yatokanayo na tozo
mbalimbali kwenye mazao ya kilimo (asilimia 20), mifugo (asilimia 15) na uvuvi
(asilimia 5) zinarudi na kutumika kuboresha sekta hizo ikiwa pamoja na
uendelezaji wa mazao ya kimkakati,” alisema.
Alitoa wito huo jana (Alhamisi, Agosti 3, 2023) wakati
akizungumza na wadau na washiriki mara baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya
Nane Nane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini
Mbeya.
Ili kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, uvuvi na
mifugo, Waziri Mkuu aliwataka wadau wa sekta hizo wazitumie taasisi za fedha
zilizopo nchini kupata mikopo itakayowasaidia kuongeza tija na kuendeleza
biashara zao.
“Taasisi za fedha zimefungua dirisha kwa ajili yenu,
wanataka wawasikie. Hakuna maendeleo bila kukopa, lakini ni lazima vigezo na
masharti vizingatiwe. Unapotaka kufanya maendeleo ukakosa mtaji, nenda kakope
lakini ukikopa mwisho wake lazima urejeshe ili na wengine waweze kukopa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea
kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za fedha ili ziweze kushusha riba
kwenye mikopo wanayotoa na kuongeza fursa kwa wajasiriamali nchini ili wapate
mikopo na kuendeleza shughuli zao ziweze kuwa na tija. “Nimefurahi sana kukuta
baadhi yao wameshusha riba mpaka asilimia tisa. Ni matumaini yangu watashuka
zaidi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa
na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa washirikiane na wizara husika
kuhakikisha vijana wanapatiwa maeneo ya mashamba, mafunzo na kuwatafutia wadau
watakaowasaidia kupata mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na
masoko ya uhakika.
“Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa mshirikiane na Mamlaka ya
Serikali za Mitaa katika maeneo yenu kuhakikisha wanatenga maeneo ili vijana
wanaopata mafunzo ya BBT (mpango wa kuwawezesha vijana kulima, kufuga na kuvua
samaki kibiashara) wakute yako tayari. Tunataka hawa vijana wakitoka kwenye
mafunzo, wakute maeneo yako tayari na waanze kazi mara moja,” alisisitiza.
0 Maoni