Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema serikali inaandaa Mfumo wa Taifa
wa uratibu na tathmini wa afua za masuala ya maendeleo ya vijana nchini
utakaosaidia kuwatambua na kuwaratibu wadau.
Kutokana na hilo, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo na
Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuzifanyia tathmini asasi za kiraia
zinazoshughulikia masuala ya vijana ili kujua utendaji kazi wake na kama
zinakidhi tija vijana.
Mhe. Katambi ameyasema hayo Agosti 3, 2023 kwenye uzinduzi
wa kongamano la vijana lililoandaliwa na asasi za kiraia 32 zinazojishughulisha
na masuala ya vijana.
“Niwaagize Katibu Mkuu na Msajili wa mashirika mfanye
tathmini ili kuhakikisha asasi hizi zinatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa
sheria na malengo ya serikali ili kuleta tija kwa vijana nchini,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana
mkoani Dodoma (DOYODO), Rajab Juma ameomba serikali kuzitengea ruzuku asasi
zinazojihusisha na masuala ya vijana kama ilivyo kwa vyama vya siasa ili
kuwafikia kundi kubwa la vijana katika kujenga kesho yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Demokrasia, Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Bret Saalwaechter ameipongeza serikali ya Tanzania
kwa ushirikishwaji wa vijana, wanawake na Watu wenye Ulemavu katika kuwaletea
maendeleo na kushughulikia changamoto zao.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Freedom House,
Daniel Lema, amesema bado kuna kundi la vijana wanashindwa kutumia fursa
zinazowazunguka ili kutengeneza kipato na kuishia kulalamika.
Kongamano hilo lomeongozwa na Kauli mbiu isemayo “Ushiriki
wa Vijana kwenye Uongozi na Utawala Bora kwa Maendeleo ya kiuchumi”
0 Maoni