TTCL yalenga kuliingiza taifa kwenye uchumi wa kidigitali

 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga, amesema shirika hilo limebeba jukumu kubwa la kulifikisha taifa katika uchumi wa kidigitali, utakaoendana na manunuzi ya bidhaa na huduma kwa mfumo wa ‘cashless’ (malipo ya fedha kidigitali).

Akizungumza na wahariri leo tarehe 24 Agosti 2023, Jijini Dar es Salaam kuhusu mwelekeo wa shirika hilo katika miaka mitano ijayo amesema, ni kujenga ubunifu wa hali ya juu katika safari ya kulipeleka taifa kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda.

“Tulikuwepo miaka 120 iliyopita, tutakuwepo miaka 120 ijayo. Tumebeba jukumu zito la kuifikisha nchi katika Uchumi wa Kidigitali,” amesema Mhandisi Ulanga.

“TTCL tunajiangalia kwa upana zaidi, sio kama shirika la kutoa huduma ndani ya nchi tu, bali shirika kubwa linaloweza kutoa huduma nje ya mipaka ya nchi, ndani ya mwaka huu tutaanza kutoa huduma yetu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),” amesema Mhandisi Ulanga.

Pamoja na mambo mengine Mhandisi Ulanga amesema, anatamani taifa lifike katika hatua ya kutotembea na pesa (cashless) na kwamba, shirika hilo ni miongoni mwa wadau katika kufikia hatua hiyo.

“Tunataka ifike mahali matumizi ya kulipa fedha ‘cash’ yasiwepo. Tutahimiza na wadau wengine tufike kwenye hatua ya cashless,” amesema Mhandis Ulanga.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mhandisi Peter Ulanga wa kwanza kushoto akifuatilia jambo pamoja na baadhi ya Wahariri katika mkutano wa kuelezea mwelekeo wa shirika hilo leo Agosti 24, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni