Serikali kupitia Taasisi zake TAWIRI na TANAPA imeendelea na zoezi endelevu la kuwarejesha mbwa mwitu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiwa ni kuhakikisha mbwa mwitu wanaendelea kuhifadhiwa katika mfumo ikolojia ya Serengeti.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuwapokea mbwa mwitu wapatao
20 waliozaliwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kuletwa Hifadhi ya Taifa Serengeti
kabla ya kuachiwa huru, Dkt. Emmanuel Masenga ambaye ni Mtafiti Mkuu na
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Serengeti amesema kuwa matokeo ya tafiti
yanaonyesha kuwa sababu kuu za kutoweka kwa mbwa mwitu katika hifadhi ya
Serengeti ni magonjwa (Rabies and Canine Distemper Virus) na ongezeko la idadi
ya simba na fisi pamoja na kuuwawa na wananchi wanapotoka nje ya hifadhi.
Aidha, Dkt. Masenga amesema jitihada za Serikali za
kuwarejesha mbwa mwitu ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ni zoezi endelevu na
lilianza tangu mwaka 2011 kwa lengo la kuhifadhi mbwa mwitu kwa ajili ya
kutunza bioanuwai na kuendeleza utalii.
Dkt. Masenga amesema kama inavyofahamika jukumu kubwa la
Taasisi ya Utafiti Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ni kufanya tafiti za
wanyamapori, hivyo TAWIRI inaendelea kufanya tafiti za kina za kuhakikisha kuwa
mbwa mwitu wanaendelea kuhifadhiwa katika mfumo ikolojia wa Serengeti.
0 Maoni