Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipo katika
hatua ya kukamilisha maandalizi ya muongozo wa kuratibu na kusimamia upangaji
na upimaji shirikishi katika Jiji la Dodoma utakaoweka utaratibu unaopaswa
kuzingatiwa katika utekelezaji zoezi hiyo.
Hatua hiyo inafuatia utekelezaji mpango wa Upimaji
Shirikishi katika jiji la Dodoma kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
kukosekana kwa uwazi katika utekelezaji wa makubaliano ya mgawanyo wa asilimia
30 kwa 70.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na
Utalii tarehe 23 Agosti 2023 mkoani Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema katika utekelezaji wa makubaliano hayo
baadhi ya watendaji wamekuwa wakitekeleza majukumu yao pasipo kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu zilizopo na hivyo kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.
"Ili kukabiliana na changamoto upangaji na upimaji
shirikishi katika jiji la Dodoma, Wizara ipo katika hatua za kukamilisha
maandalizi ya mwongozo wa kuratibu na kusimamia upangaji na upimaji Shirikishi," alisema Dkt Mabula.
Ameeleza kuwa, wizara yake inaendelea na utekelezaji wa
mpango wa upimaji shirikishi ulioanzishwa ili kuongeza kasi ya upangaji na
upimaji wa ardhi katika jiji la Dodoma baada ya Serikali kuhamishia shughuli
zake jijini Dodoma julai 2016.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, hali hiyo ya Serikali kuhamia
Dodoma imesababisha kuongezeka kwa mahitaji makubwa ya ardhi iliyopangwa na
kupimwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Akielezea zaidi kuhusiana na Program ya Urasimishaji Makazi
yasiyopangwa nchini, Waziri huyo wa Ardhi aliweka bayana kuwa, kupitia program
hiyo jumla ya vipande vya ardhi 2, 480,165 vimetambuliwa ambapo kati ya hivyo
viwanja 2,474,329 vimepangwa na kurasimishwa, viwanja 1,264,855 vimepimwa na
kuidhinishwa na viwanja 1,114,296 upimaji wake haujakamilika.
Aidha, alisema hadi kufikia julai 31, 2023 jumla ya ankara
za umilikishaji wa viwanja vya urasimishaji 601, 076 zimetolewa ambapo kati ya
hizo jumla ya hatimiliki 203,290 zimeandaliwa.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Dkt Mabula alisema,
program ya urasimishaji makazi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
mwitikio hafifu wa wananchi kuchangia gharama za upimaji na umililkishaji hali
inayosababisha miradi kutotekelezwa kwa wakati.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Malisili na Utalii
mbali na kuipongeza wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi
kubwa inayofanya lakini wameitaka kujipanga na kuongeza kasi ya umilikishaji
ardhi huku ikihakikisha inasambaza vifaa vya kutosha kwenye ofisi zake.
"Kazi inafanyika lakini ukiangalia bado changamoto ni kubwa
hivyo mnatakiwa kuongeza kasi na kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri kwa
mfano mtu anaanza kujenga nyumba na inafikia hatua kubwa halafu anaambiwa
amejenga bila kufuata taratibu hii siyo sawa," alisema Makamu Mwenyekiti wa
Kamati Najma Giga.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepangiwa
kuwasilisha mbele ya kamati taarifa mbalimbali kama vile utendaji wa Tume ya
Taifa ya Matumizi ya Ardhi, utekelezaji program ya kupanga, kupima na
kumilikisha ardhi, utekelezaji program ya urasimishaji makazi yasiyo pangwa
nchini, utekelezaji wa mpango wa upimaji shirikishi katika jiji la Dodoma
pamoja na utatuzi wa changamotio za upimaji ardhi nchini mbalimbali.
0 Maoni