Nyota wa filamu wa China kutangaza utalii wa Tanzania nchini kwao

 

Rais Samia Suluhu Hassan, amempa cheti cha hadhi maalum staa wa filamu kutoka nchini China, Jing Dong, kuwa Balozi wa Heshima wa Utalii ili kusaidia kuitangaza Tanzania katika Taifa hilo lenye watu takribani Bilioni 1.4, huku Wachina takribani milioni 200 wakisafiri kwenda kutalii sehemu mbalimbali duniani kila mwaka.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana jioni kutoka jijini Arusha ambako Mhe. Rais Samia yupo kwa majukumu mbalimbali ya Kiserikali, imesema Bw. Jing Dong amepokea heshima hiyo alipokutana na Rais kwa mazungumzo katika kikao kilichohudhuriwa pia na Waziri wa Utalii, Mohammed Mchengerwa.

Viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) ni Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Tanapa, Jenerali Mstaafu George Waitara, Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Balozi Dkt. Ramadhan Dau na watendaji wengine waandamizi.

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Bw. Jing Dong ni miongoni mwa madtaa 100 nchini China, akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 200, tuzo zaidi ya 10 zikiwemo za China Golden Lion Award for Drama (2012) ambayo ni tuzo ya juu kuliko zote katika eneo la tamthilia za kwenye TV na Msanii Bora wa Kiume wa China na Msanii Bora wa Televisheni (kupitia filamu za Surgeons na The First Half of My Life ambazo pia ziliongoza kwa mauzo nchini humo na kuwa maarufu sana miongoni mwa Wachina).

Mwaka 2018 alishinda Tuzo iliyowashindanisha mastaa wa China walioko China na Marekani na kushinda kuwa Msanii Bora wa Kiume (Chinese American Film Festival: Best Actor kupitia filamu ya Mr. Right) na anatajwa kuwa mmoja wa wasanii wa China maarufu na mabilionea kutokana na kazi yao hiyo.

Baadhi ya filamu na tamthilia zake mashuhuri ni: Nirvana in Fire (2015), “Ode to Joy” (2016), “Candle in the Tomb” (2016-2017), “Surgeons” (2017), “Mr. Right” (2018), The People's Property (2019), If Time Flows Back (2019) and The Best Partner (2020).

Nyingine ni: Legend of Entrepreneurship (2012), The Disguiser (2015), Candle in the Tomb (2016), Surgeons (2017) and The First Half of My Life (2017).

Chapisha Maoni

0 Maoni