Mchengerwa: Watanzania wajitokeze kuona uvukaji wa nyumbu

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) amewataka Watanzania kuwa na mwamko na kujitokeza kwa wingi kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania ikiwemo Serengeti kushuhudia maajabu yaliyopo.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo akiwa Kogatende, katika Hifadhi ya Taifa Serengeti baada ya kushuhudia tukio kubwa na la kipekee duniani la uvukaji wa nyumbu Mto Mara pamoja na wanyama wengine.

"Nawaasa na kuwakaribisha watanzania kuja kujionea wao wenyewe uvukaji wa nyumbu mubashara. Hili tukio ni la kipekee na la kihistoria," alisema Waziri Mchengerwa.

Akiongea akiwa na Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu Kamishna Benedict Wakulyamba, wajumbe wa Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii, wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Timotheo Mnzava na watumishi wa wizara, amewapongeza wahifadhi wote nchini kwa jitihada zinazofanywa na watumishi hao haswa watumishi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuwataka kutokukata tamaa.

" Nawapongeza sana kwa jitihada mnazofanya fanyeni kazi kwa bidii na kwa kujituma bila kukata tamaa na wala bila kumwonea mtu. Kazi mnayofanya ni nzuri fanyeni kazi kwa kufuata kanuni, sheria, taratibu na maadili," alisema Mhe. Mchengerwa.

 Aidha, Mhe. Mchengerwa alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha harakati za kuitangaza nchi yetu kupitia filamu ya The Royal Tour.

"Takwimu zinaonyesha idadi ya watalii imeongezeka, kwa mfano katika mwaka wa fedha 2022/2023 tulipata zaidi ya watalii milioni 1.6. Matarajio ya wizara ni kiwango hiki kuongezeka zaidi," alisema Waziri Mchengerwa.

Pia, aliwasifia watumishi wa TANAPA kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti kushinda tuzo mara nne mfululizo na kuiwezesha kujulikana kimataifa, kuwa miongoni mwa maajabu saba ya dunia pamoja na kuwa na wanyama wengi na wakubwa.

Tukio hili linaloshangaza na kuvuta hisia za watalii wengi duniani la Nyumbu na Pundamilia kuvuka Mto Mara hufanyika kila mwaka kuanzia mwezi Agosti hadi katikati ya mwezi Septemba.

Na. Brigitha Kimario - Serengeti

Chapisha Maoni

0 Maoni