Mchengerwa, Wabunge waongoza wageni kushuhudia msafara wa nyumbu

 

Waziri wa Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa, Wabunge waongoza wageni kushuhudia msafara wa nyumbu ambao ni tukio kubwa duniani linalojulikana kwa lugha ya Kingereza kama Serengeti Grand Migration na #NiSerengetiTena.

Katika tukio hilo la kwanza na la aina yake lililofanyika kwenye eneo la Kogatende, Serengeti, wageni mbalimbali kutoka mataifa mengi waliungana na viongozi hao wakishuhudia kwa zaidi ya saa 2 wanyama aina ya nyumbu wakisindikizwa na pundamilia wakivuka na kupitia majaribu mbalimbali ikiwemo kukabiliana na mamba kwenye Mto Mara.

Pamoja na Waziri wa Utalii Mhe. Mohammed Mchengerwa, Naibu wake, Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Benedict Wakulyamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe Timotheo Mnzava aliongoza baadhi ya wajumbe wa Kamati hizo kushuhudia tukio hilo la kihistoria na kubaki wakishangazwa na maajabu hayo.

“Ndio tumeanza kutekeleza mikakati kabambe ya kuutangaza utalii wetu. tukio hili ni la kihistoria na huwezi kulikuta popote duniani; ujio wetu hapa ni kukipa heshima na kulitangaza zaidi duniani,” alisema Waziri Mchengerwa.

“Tumejionea maajabu leo na tunaipongeza Serikali na wahifadhi wetu kwa kuwalinda wanyama hawa mpaka leo tumejionea tukio hili la aina yake,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Mnzava.

Waziri wa Utalii Mhe. Mohammed Mchengerwa aliyesimama akitumia kionambali kuangalia msafara mkubwa wa nyumbu wanyama aina ya nyumbu wakisindikizwa na pundamilia wakivuka na kupitia majaribu mbalimbali ikiwemo kukabiliana na mamba kwenye Mto Mara.

Chapisha Maoni

0 Maoni