Kamati ya Bunge yaelezwa umuhimu wa Maafisa Ustawi wa Jamii

 

Serikali imesema Wataalam wa Ustawi wa Jamii ni muhimu katika Maendeleo ya Jamii kuanzia kwenye kuimarisha Malezi na Makuzi ya Mtoto.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akijibu hoja mbalimbali za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii katika Kikao cha kupokea taarifa ya mafanikio na changamoto za Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Kijitonyama na Kisangara) jana jijini Dodoma.

Waziri Dkt Gwajima amesema Huduma za Ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika kusaidia kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za ukatili kwenye familia na jamii.

"Kitovu chetu katika masuala ya Ustawi wa Jamii ni Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Kijitonyama na Kisangara) hivyo tutaweka mikakati thabiti ya kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wahitaji wengi katika jamii," amesema Waziri Dkt. Gwajima

Amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii huku ikijadili na Wadau kuhusu umuhimu na uwezekano wa kila Taasisi au Kampuni kutenga ajira za Maafisa Ustawi wa Jamii Ili kwenda na wakati wa sasa ambapo shughuli za maendeleo ya kiuchumi pia zinakuja na changamoto za msongo (stress) zinazohitaji huduma za ustawi.

"Ni wakati muafaka kwa huduma hizi ziwepo katika jamii ili wananchi waache kuwaza kuwa wanaumwa malaria kumbe inawezekana mtu ana msongo wa mawazo hivyo anahitaji Elimu ushauri na msaada wa kisaikolojia," amesema Dkt. Gwajima

Akisoma taarifa ya mafanikio ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Kijitonyama na Kisangara) Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Joyce Nyoni amesema Taasisi kwa mwaka 2023 inatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake hivyo wanajivunia kwa kuzalisha wataalamu wa Ustawi wa Jamii wanaotumika kujenga jamii na Taifa lenye ustawi.

Ameeleza kuwa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano imefanikiwa kuboresha miundombinu ya Taasisi ikiwemo kujenga na kukarabati kumbi za mihadhara, Ofisi na nyumba za watumishi na miundombinu mingine wezeshi kwa wanafunzi na watumishi wa Taasisi hiyo.

"Taasisi katika kuboresha utoaji wa elimu tumeweza kuwawezesha watumishi 50 kujiendeleza katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu na Uzamili na pia kuajiri wahadhiri 52 kwa mwaka wa fedha 2022/23," amesema Dkt. Nyoni.

Ameendelea kuyataja mafanikio ya Taasisi hiyo ni kutoa huduma za unasihi na kisaikolojia kwa kuanzisha Kituo cha Elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia pamoja na Dawati la Jinsia iliyosaidia kutoa huduma kwa jamii katika maeneo mbalimbali.

Dkt. Nyoni amesema Taasisi imefanikiwa kupata tuzo mara tatu inayotolewa na Bodi ya Wakaguzi na Wahasibu (NBAA) kwa uaandaji Bora wa hesabu pia wamefanikiwa kuwawezesha wahadhiri wao kuongeza utaalam kwa ngazi ya Shahada ya Uzamivu na Uzamili katika Vyuo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii Mhe. Fatma Toufiq ameitaka Wizara kuendelea kutoa taarifa muhimu za Taasisi na Idara zake ili wajumbe wazidi kujenga uelewa zaidi na kubeba vema zaidi ajenda mbalimbali za ustawi wa jamii katika mikakati na Bajeti za Serikali. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ameishukuru Kamati hiyo kwa kupokea taarifa na kuahidi kuendelea kuhakikisha Kamati inaifahamu vema zaidi taasisi hii na Dira yake baada ya miaka 50.

Kamati ya Kudumu ya Bunge na Ustawi wa Jamii ipo katika wiki ya kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Chapisha Maoni

0 Maoni