Jeshi lawaonya wanaouza na wanaovaa sare zinazofanana na za JWTZ

 

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeonya tabia iliyoanza kuibuka kwa siku za hivi karibu ya wimbi kubwa la wananchi wanaovaa sare zinazofanana na za JWTZ ama mavazi yanayofanana na sare za kijeshi.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, amesema kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya wananchi wanaokamatwa au konekana wakiwa wamevaa sare za JWTZ ama mavazi yanayofanana na sare za kijeshi.

"Nimewaita waandishi wa habari leo ili kupitia kwenu JWTZ liweze kutoa taarifa kuhusiana na kadhia hiyo inayokizana na katazo la kisheria la raia kuvaa, kumiliki au kuuza mavazi ya kijeshi au yanayoelekea kufanana na sare za jeshi," alisema Luteni Kanali Ilonda.

Amesema kwamba sheria inakataza mavazi hayo ambayo ni pamoja na kombati (vazi la mabaka mabaka), makoti, t-sheti, suruali, magauni, kofia, viatu, mabegi na kaptura zenye rangi zinazofanana ua kushonwa katika mitindo ya kijeshi.

Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, amesema kwamba katazo hilo ni kwa mujibu wa kifungu cha 99 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa (NDA) sura ya 192 Sheria namba 24 ya mwaka 1966 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Ameongeza kwamba, kifungu cha 178 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 (Penal Code) na kifungu cha 6 cha Sheria ya Usalama wa Taifa, vinakataza raia kuvaa sare na mavazi ya majeshi ya ulinzi au yanayofafana nayo.

Amesema kwamba zipo baadhi ya taasisi zinazowashonea watumishi wake sare za aina hiyo na wapo pia baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa raia kupitia maduka yao ama maeneo yao ya biashara.

Ameeleza kuwa wapo pia baadhi ya wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu. Pia, amesema wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiyatumia kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria na kudhaniwa kuwa ni wanajeshi.

Chapisha Maoni

0 Maoni