Serikali imewaonya wamiliki wa makao ya kulea watoto nchini
waliogeuza makao hayo kujinufaisha kwa misaada mbalimbali inayotolewa hasa ya
fedha.
Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu alipotembelea Kijiji
cha Matumaini kinacholea watoto jijini Dodoma, jana.
Dkt. Jingu amesema kuwa baadhi ya wamiliki wa Makao ya kulea
watoto wamekuwa wakifanya hivyo na hata kupiga picha za watoto kwa ajili ya
kupata misaada ambayo haiwafikii wahusika na fedha zinazotolewa na wafadhili
wenye mapenzi mema huzitumia kujinufaisha.
"Mnaotumia Makao ya Watoto kujinufasha tunawamulika,
tutawafuatilia na tutawachukulia hatua kali kwa sababu mnakiuka Sheria na
taratibu zilizopo. Huu ni wizi na ukatili dhidi ya Watoto na tunawahujumu
waliotoka hiyo misaada," alisisitiza Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa mtoto anatakiwa kulelewa na kutunzwa
katika familia na jamii ila ikitokea mtoto amepata changamoto za maisha na
kujikuta yupo katika mazingira ambao anakosa Malezi katika familia ndipo Makao
yanatumika kuwalea.
"Mpaka sasa kuna jumla ya Makao ya kulea watoto 341
ambayo yanatoa huduma ya kulea watoto waliopatwa na changamoto zilizosababisha
kutolelewa katika familia," alisema Dkt. Jingu
Pia, ameyataka Makao ya kulea Watoto nchini kuzingatia suala
la Malezi hasa katika tamaduni na maadili ya kitanzania ili kujenga watoto
walio na maadili mema hivyo kujenga taifa lenye maadili.
"Makao ya watoto sio biashara bali ni sehemu ya
kuwasaidia watoto ambao hawajapata fursa za kulelewa katika familia, ni njia
mbalada ya malezi kwa watoto wetu," alisema Dkt. Jingu
Vilevile amewataka wamiliki wa Makao ya Watoto ambao
wameshindwa kuendesha Makao hayo wasing'ang'anie kukaa na watoto bali watoe
taarifa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii walipo katika maeneo yao ili watoto hao
wapate sehemu nyingine watakazopata malezi.
Aidha, Dkt. Jingu ameupongeza uongozi wa Makao ya kulea
watoto ya Kijiji cha Matumaini kwa kazi nzuri ya kuwalea na kuwatunza watoto
waliopo katika Makao hayo kama watoto walio katika familia zao kwa kufuata
Sheria na taratibu za uendeshaji wa Makao ya kuelea Watoto nchini.
Akisoma taarifa ya Kijiji cha Matumaini mmoja wa walezi wa
Makao hayo Sister Euphrasia Julius amesema kuwa Malezi ya Watoto katika Makao
hayo ni ya Wana ndoa na kifamilia wa kujitolea kuwalea watoto bila kuwaasili
kwa muda wakakaopenda ili watoto hao waweze kupata Malezi ya Baba na Mama kama
watoto wengine katika familia.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt.
Nandera Mhando amesema lengo ya kutembelea Makao ya Watoto ni kuangalia
utendaji kazi wake na mazingira wanayolelewa Watoto kama yanakidhi vigezo,
kanuni, miongozo, Sheria na madhumuni ya uanzishaji wa Makao ya kulea watoto.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum ipo katika ufuatiliaji wa Makao ya kulea watoto
ambayo hayafuati Sheria na taratibu za uendeshaji wa Makao hayo nchini na
itachukua Sheria kwa wamiliki wote ambao watabainika kufanya vitendo hivyo.
Na. Raymond Mushumbusi WMJJWM Dodoma
0 Maoni