Bandari ya Dar es Salaam yavuka malengo ya kuhudumia mizigo

 

Bandari ya Dar es Salaam imehudumia mizigo ya tani 21,271,000 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2023, na kuvuka lengo iliyowekewa na Serikali la kuhudumia mizigo tani 19,600,000, ambapo kwa mwaka 2020-2021 ilihudumia tani milioni 18.

Mafanikio hayo yametokana na mpango wa kuendeleza bandari ya Dar es Salaam, ulioanza mwaka 2017, ambao pamoja na mambo mengine umefanikisha kukamilika kwa ujenzi wa gati namba sifuri pamoja na miundo mingine ya bandari hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari leo Julai 21, 2023 Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Seleiman Mrisho, amesema shughuli za bandari hiyo zimekuwa zikichangia kati ya asilimia 37 hadi 40 ya mapato ya kikodi na forodha.

“Ukifanya upembuzi utabaini katika mwaka ulioishi Juni 2023, bandari ya Dar es Salaam imehudumia mizigo nchi jirani chini ya tani milioni 10, wakati soko la nchi jirani saba ni zaidi ya tani milioni 70 kwa mwaka,” alisema Mrisho na kuongeza, “Hii inamaanisha kuwa pamoja na maboresho tuliyoyafanya bado hayajasaidia kukidhi mahitaji ya soko la nchi jirani ndio maana tunasema bandari ya Dar es Salaam inahitaji uwekezaji”.

Amesema katika mwaka unaoishi Juni 2023 bandari ya Dar es Salaam imehudumia mizigo tani milioni 3.5 tu ya soko la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambalo kwa mwaka mahitaji yake ni tani milioni 21, na kwa mizigo ya Uganda wamehudumia chini ya asilimia tatu ya mizigo yote.

Bw. Mrisho amesema mazingira ya kijografia yanaifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa na nafasi kubwa ya kutumika na nchi jirani katika kuhudumia mizigo, “Soko tayari lipo, watumiaji wapo, wasafirishaji na waagizaji mizigo wapo, tatizo ni changamoto za bandari”.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara, wahariri walielezwa kuwa kwa sasa bandari ya Dar es Salaam inamagati 12 tu, ikilinganishwa na bandari ya jirani zetu ya Mombasa, Kenya yenye magati 26.

Kwa upande wake Mhandisi Kijavara amesema kwamba Serikali inampango wa kuongeza ujenzi wa magati ya bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga magati ya ziada matano kwa kuazia mwaka huu itajengwa gati ya kwanza ya mita 300 na kuendelea hadi kufikia magati 5.

“Tunatarajia kuanza ujenzi wa gati la kwanza mwaka huu ambalo makadirio yake yanatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 3, ukiangalia kiasi hicho cha fedha ndio maana sisi tunasema tuhahitaji uwekezaji,” amesema Mhandisi Kijavara.

Pia Mhandisi Kijavara amesema kwamba katika mwaka huu utaanza mchakato wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, “tunatarajia mwezi wa tisa kupata mkadarasi na ujenzi wake nao utaanza mwaka huu ili kuongeza wigo mpana wa kuhudumia mizigo nchini”.

Chapisha Maoni

0 Maoni