Waziri Mkuu Majaliwa amaliza mgomo Kariakoo atoa agizo kwa TRA

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasihi wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kuendelea na biashara zao wakati serikali ikitafutia ufumbuzi wa kero zao.


Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito huo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo ambao wamekuwa katika mgomo kwa zaidi ya saa tisa “ hata kama kuna matatizo bora shughuli zikawa zinaendelea ili tusiendelee kuwapoteza wateja wetu kutoka nje na ile hadhi ya kimataifa iweze kuendelea.” 


Hata hivyo amesitisha utaratibu wa Kamata kamata huku akieleza inachangia kuua biashara na maduka mengi yatafungwa. “Mfanyabiashara anadaiwa kodi, mpelekee notisi, na kama kweli ameridhia kufanya biashara na anajua ukifanya biashara ni lazima ulipe kodi, atalipa kodi ili afanye biashara.” amesema 


“Tunaheshimu kazi zenu, tunatambua mchango wenu kwenye uchumi wa nchi hii na tutaendelea kuunga mkono mchango wenu wa uchumi kwenye nchi hii.” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa 


Kwa upande mwingine amemtaka Kamishna wa TRA kusitisha tozo ya maghala na kumtaka aanze na utoaji wa elimu na baadae kuweka utaratibu wa ukusanyaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabishara wa Soko la Kariakoo Martin Mbwana amesema wamekubali kufungua maduka na kuendelea na biashara kama kawaida.


Amesema wamefikia uamuzi huo baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufika katika soko hilo kutatua na kuahidi kuendelea kutatua changamoto zilizowapelekea kuitisha mgomo ulioanza leo Mei 15, 2023 asubuhi.

Chapisha Maoni

0 Maoni