Sheria mpya ya habari Zanzibar yakamilika kwa asilimia 80

 


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imesema kuwa mchakato wa kupata sheria mpya ya habari Zanzibar umekamilika kwa asilimia 80, hivyo basi muda si mrefu sheria hiyo itakamilika.

Kauli hiyo imetolewa leo Zanzibar na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita wakati akifungua Maonesho na Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

“Kila unapoenda kwenye mikutano ama kwenye majadiliano ya waandishi wa habari unasikia kilio ni sheria sheria sheria, niwahakikishieni serikali ya awamu ya nane ni sikivu na itawaleteeni sheria bora,” amesema Mhe. Tabia.

Mhe. Tabia amewataka waandishi wa habari pamoja na wadau wa habari kuwa na imani na serikali ya Zanzibar na kuacha kuitisha sheria hiyo kuangaliwa kila mara jambo linalochelewesha mchakato.

“Muiamini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tumeandaa sheria nzuri, tumeangalia sheria mbalimbali upande wa bara na za nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kuja na sheria iliyobora kabisa,” amesema Wazairi Tabia.

Mhe. Tabia amesema serikali zote mbili ya Zanzibar na Tanzania zimedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo kwa kasi, kukuza uchumi na kuendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari.

Aidha, Mhe. Tabia ameahidi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea kushirikiana na UNESCO ambaye ni mfadhili kiongozi wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa zaidi ya miaka 30 bila kuchoka.

Chapisha Maoni

0 Maoni