Mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo huenda ukaendelea kwa
siku kadhaa licha ya jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla
kuingilia kati hii leo kujaribu kuutuliza, lakini inaonekana jitihada hizo
zimegonga mwamba.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makalla amekutana na
wafanyabiashara hao na kuwataka kusitisha mgomo huo, lakini wafanyabiashara huenda
wakaendelea na mgomo huo hadi Ijumaa, sasa wakitaka kukutana na Rais Dk. Samia
Suluhu Hassan.
Mgomo huo wa wafanyabiashara wa Kariakaoo umenza leo
jumatatu, ambapo wamefunga maduka yao kwa ajili ya kushinikiza serikali
kuingilia kati utitiri wa kodi wanaotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Msimamo wa kuendelea na mgomo huo, umeonekana kwenye kikao
na Mkuu wa Mkoa Makalla ambapo walionekana kutoridhika na maelezo yake, na hata
aliposema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atafanya kikao na kamati ya
wafanyabiashara wa soko hilo siku ya Alhamisi Dodoma.
Baadhi ya wafanyabiashara wamesema iwapo wanataka wafungue
maduka na kufanya biashara ni vyema watimize lengo lao la kukutana na Rais
Samia Suluhu Hassan ili wamueleze madhili wanayopitika wafanyabiashara na si mkuu
wa mkoa.
Iwapo msimamo huo wa mgomo utaendelea hadi Ijumaa utasababisha
athari za kiuchumi, kutokana na eneo hilo la Kariakoo, kuwa ni kitovu cha
biashara nchini, likitegemewa zaidi na mikoa mingine na hata wafanyabiashara
kutoka nchi za jirani.
Naye Mjunbe wa Jumuiya ya wafanyabiashara Honest Kalisti amesema
hakuna kurudi nyuma katika mgomo huo, hadi hapo kilio chao kitakaposikilizwa na
kutatuliwa huku akisema hili wanalolalamikia Waziri Fedha na Mipango Dk. Mwigulu
Nchemba analijua na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa analijua.
0 Maoni