Serikali yadhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Marburg

 


Wizara ya Afya imesema kwamba taarifa za kitabibu zinaonesha kuwa kuanzia tarehe 21 Aprili mwaka huu Tanzania imedhibiti ugonjwa wa Marburg na hakuna mgonjwa yeyote mwenye virusi vya ugonjwa ugonjwa huo mkoani Kagera.

Hayo ameyasema leo Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu alipokuwa anaongea na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za wizara hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.

“Wagonjwa wawili waliokuwa wamesalia katika vituo maalum vya matibabu waliruhusiwa kutoka tarehe 20 na 21 Aprili 2023 baada ya kuthibitika kimaabara kuwa hawana tena virusi vya Marburg,” alisema Waziri Ummy.

Amesema hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali zilipelekea kuhakikisha ugonjwa huu wa Marburg hausambai nje ya familia zilizoathirika na kwa watumishi wa afya waliowahudumia wagonjwa kabla ya kuthibitika uwepo wa ugonjwa huo. 

Pamoja na mambo mengie, Waziri Ummy amesema kuwa tangu uwepo wa ugonjwa huo ulipotangazwa jumla ya watu waliopata maambukizi ni tisa kati ya hao watatu wamepona na wagonjwa sita walipoteza maisha.

Miongoni mwa waliopona ni pamoja na daktari aliyewahudumia wagonjwa wa mwanzo kabla ya kuthibitika, miongoni mwa watu waliopoteza maisha ni pamoja na mtumishi mmoja wa afya na mtoto mwenye umri wa miezi tisa.

Hata hivyo amesema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa Marbug.

“Iwapo hakutatokea mgonjwa mpya mwenye virusi vya Marburg baada ya siku 42 yaani hadi ifikapo tarehe 31 Mei 2023 ndipo tutatangaza rasmi kumalizika kwa ugonjwa huu,” amesema Waziri Ummy.

Chapisha Maoni

0 Maoni