Mhubiri akiri watu 15 kufa kanisani kwake

 


Mhubiri wa Mombasa nchini Kenya Ezekiel Odero amekiri kuwa watu 15 walikufa wakijaribu kupata tiba ya kiroho katika kanisa lake la New Life Prayer Centre, katika kipindi cha mwaka mmoja na mwezi mmoja.

Kupitia mawakili wake Cliff Ombeta, Danstan Omari na Shadrack Wamboi. Odero amesema watu hao 15 waliomba msaada wake wakiwa mahututi.

“Katika mwaka mmoja na mwezi mmoja wakati kanisa hilo likiendesha shughuli zake watu 15 tu wamekufa katika eneo la kanisa la Mchungaji Ezekiel,” alisema wakili Omari.

Wakili huyo amesema kwamba kanisa hilo linasera inayotaka wagonjwa wanaofika kwa maombi lazima waambatane na ndugu zao, la sivyo mgonjwa hatapokelewa kwa maombi.

Mawakili hao wa mhubiri huyo wameongea hayo nje ya kituo cha Polisi cha kaunti ya Mombasa baada ya kujiunga na upande wa kumtetea Odero.

Mchungaji Odero anaendelea kushikiliwa na polisi, ambapo hapo jana Ijumaa alifikishwa mahakamani.

Mhubiri Odero anachunguzwa kwa mauaji, kusaidia watu kujiua, utekaji, kueneza itikadi kali, mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili kwa watoto, wizi wa fedha, utakatishaji fedha na kusaidia utekelezaji uhalifu.


Chapisha Maoni

0 Maoni