NECTA yavifungia vituo viwili, mitihani kidato cha sita kuanza Mei pili

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limevifungia vituo viwili vya mitihani ambavyo ni Shule Sekondari Thaqaaf iliyoko Mwanza na Twibhoki iliyoko Mara baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uendeshaji mitihani ya CSEE mwaka 2022.


Aidha baraza hilo limesema wanafunzi 337 waliofutiwa mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE)  mwaka 2022, watafanya mitihani hiyo pamoja na wanafunzi wa kidato cha sita kuanzia Mei 2 hadi 15, mwaka huu na kwamba maandalizi ya mitihani hiyo ya marudio imekamilika na itaanza Mei 2 hadi Mei 15.


Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 30, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Said Ally Mohamed amesema pamoja na kufungia vituo hivyo, baraza lilijiridhisha Shule za Sekondari Thaqaaf na Twibhoki zilifanya ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa mitihani.


"Baraza limefungia vituo hivi kwa mujibu wa kifungu cha 4(8) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 hadi tutakapojiridhisha kuwa ni vituo salama kuendesha mtihani wa kitaifa," alifafanua.


Vituo vilivyobainika awali kuhusika katika udanganyifu huo na kutangazwa kufungiwa kuwa vituo vya mitihani ni Shule za Sekondari Cornelius na Andrew Faza Memorial zilizopo Dar es Salaam na Shule ya Sekondari Mnemonic Academy iliyopo Zanzibar," alisema Dk.Mohamed.

Chapisha Maoni

0 Maoni