Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben kwagilwa amesema Watanzania takriban milioni 6 wananufaika na Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi ambayo pia inachangia pato la taifa kwa asilimia 2.2.
Amesema hayo wakati kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Nadra Ghulam Rashid aliyetaka kujua Serikali mbili za Muungano zina mkakati gani wa pamoja katika utekelezaji wa Sera ya Uchumu wa Buluu ambao ni nguzo kubwa ya kubadilisha uchumi wa nchi.
Aidha, Mhe. Kwagilwa alisema Serikali kupitia Mifuko mbalimbali inawasaidia wanawake kwenye vikundi au mtu mmoja mmoja na kwamba hivi sasa kuna mradi wa takriban dola milioni 150 za mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa katika halmashauri 65 zilizopo nchini zikiwemo 11 kutoka Zanzibar.
Alieleza kuwa kutokana na kuendelea kukua kwa sekta hiyo, Tanzania imepiga hatua kikanda na kimataifa ambapo Oktoba 06 hadi 09, 2026 itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12) ambao utajadili masuala ya utunzaji na uendelezaji wa Bahari ya Hindi.
Alisema hadi sasa, Serikali ya Jammhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kushirikiana katika maandalizi ya mkutano huo mkubwa ikiwa ni pamoja na kuratibu ushiriki na shughuli mbalimbali zinazohusiana na Uchumi wa Buluu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti hatua za ushirikiano huu zinalenga Hatua kuimarisha uratibu na kuhakikisha utekelezaji wa Uchumi wa Buluu unafanyika kwa mtazamo wa pamoja, kwa kuzingatia majukumu ya kila Serikali,” alisisitiza Mhe. Kwagilwa.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema Serikali zote mbili za Muungano zinaendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Sera ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar ya mwaka 2022, pamoja na mikakati na mipango yake ya utekelezaji.
Alibainisha kuwa katika kutekeleza Sera hizo, serikali zote mbili zimeendelea kutekeleza mikakati ya pamoja ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Uchumi wa Buluu ikiwemo uratibu wa masuala ya uchumi wa buluu, kuandaa Mpango wa Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Maji, kuelimisha wananchi na kuratibu mikataba, itifaki na maazimio ya kimataifa na kikanda yanayohusiana na sekta hiyo.
Sera hizo zimekuwa zikitekelezwa kupitia Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024–2034 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar wa mwaka 2022–2027.
Aidha, katika kuratibu utekelezaji wa mikakati hiyo, Serikali mbili zimeendelea kushirikiana katika kuandaa kwa pamoja Mwongozo wa Uchumi wa Buluu na kufanya uainishaji wa pamoja ili kubaini maeneo ya kipaumbele, fursa na changamoto zinazohitaji ushirikiano.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kwagilwa amesema Serikali imeweka utaratibu wa kufungua fursa kwa vijana wa pande zote mbili za Muungano kwa kuwawezesha rasilimali fedha kwa ajili ya kushiriki katika miradi ya uvuvi, kilimo kupitia uchumi wa buluu.
Alisema hayi wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Magomeni Mhe. Imamu vuai aliyetaka kujua Serikali imeweka mikakati ipi kuhakikisha vijana hasa katika maeneo ya pwani wananufaika na uchumi wa buluu.

0 Maoni