JAB yakutana na timu ya Good Morning Wasafi FM

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imekutana na kufanya mazungumzo na watangazaji na waandaaji wa kipindi cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi FM, ambapo imewakumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kikao hicho kimefanyika leo, Septemba 2, 2026, katika Makao Makuu ya JAB, Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam, kikilenga kuimarisha uelewa wa watangazaji hao kuhusu misingi ya weledi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya majukwaa ya habari.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amefafanua matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229; Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306; pamoja na kanuni zake zinazopaswa kuzingatiwa katika utayarishaji na utangazaji wa maudhui.

Wakili Kipangula ameeleza kuwa kuzingatia sheria na maadili ni msingi wa kulinda heshima ya taaluma, haki za watu wanaohusika katika maudhui na imani ya jamii kwa Waandishi wa Habari.

Baada ya mazungumzo hayo, watangazaji wakongwe Gelard Hando na Hilary Mtuta, maarufu kama Zembwela, walikabidhiwa vitambulisho vyao vya ithibati ya uandishi wa habari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.

Makabidhiano hayo yamekamilisha hatua ya kuwatambulisha rasmi kama Waandishi wa Habari wenye ithibati, wenye wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, maadili na uwajibikaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni