Wananchi 554 kulipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara wilayani Mbogwe

‎Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 554 wanaoathiriwa na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 58 kwa kiwango cha lami wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.‎

‎Zoezi hilo linahusisha wananchi ambao mali zao ikiwemo nyumba, mazao na maeneo mengine zimeathiriwa na utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Mbogwe.‎

‎Akizungumza wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa TARURA wilaya ya Mbogwe Mhandisi Patrick Chacha amesema tathmini ya mali za wananchi wanaoathiriwa na mradi imefanyika kwa lengo la kuhakikisha wanapata stahiki zao kabla ya kupisha utekelezaji wa mradi.‎

‎Mhandisi Chacha amesema ulipaji wa fidia ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mradi kwani unalenga kuwawezesha wananchi wanaoathiriwa na mradi kurejesha maisha yao na kuendelea na shughuli zao baada ya kupisha ujenzi wa barabara.‎

‎"Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi hiki cha fedha ili kuwezesha wananchi kujenga nyumba mpya na kuendelea na maisha yao baada ya kuondolewa makazi yao ya awali kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara," amesema Mhandisi Chacha.‎

‎Aidha, Mhandisi Chacha amesema wilaya ya Mbogwe ni miongoni mwa maeneo yatakayopata manufaa makubwa kutokana na mradi huo akieleza kuwa ujenzi wa kilomita 58 kwa kiwango cha lami utaboresha usafiri na usafirishaji, huku ukifungua fursa mpya za biashara na kuongeza thamani ya shughuli za kiuchumi kwa wananchi.‎

‎Amesema barabara hizo zitakapokamilika zitasaidia kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na mazao, kupunguza changamoto za usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.‎

‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Kabanga Bw. Joseph Masanja amesema zoezi la tathmini ya mali za wananchi katika eneo lake limefanyika kwa ufasaha huku wananchi wakieleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuhakikisha wanapata fidia zao.‎

‎Masanja amesema awali baadhi ya wananchi walikuwa na mashaka kuhusu uwezekano wa utekelezaji wa mradi huo lakini hatua iliyofikiwa sasa imewapa matumaini makubwa.‎

‎"Mwanzoni watu walidhani suala hili haliwezekani lakini sasa tumefikia hatua ya mwisho ya kulipwa fidia na kila mmoja wetu anapongeza jitihada za serikali," amesema.‎

‎Ametoa wito kwa wananchi wa Kabanga na maeneo mengine ya Mbogwe kutumia fursa zitakazojitokeza baada ya kukamilika kwa mradi huo hususan katika biashara, kilimo, usafirishaji na huduma mbalimbali.‎

‎Mradi wa ujenzi wa barabara hizo unatekelezwa na TARURA kupitia mradi wa RISE unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.



Chapisha Maoni

0 Maoni