Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde amekutana na wakurugenzi wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited mjini Dodoma kujadili maendeleo ya Mradi wa Mkuju River unaohusisha uchimbaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Akiongoza ujumbe wa kampuni hiyo jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Vladislav Shulga, amesema Mantra Tanzania Limited ipo tayari kuendelea na ujenzi wa mradi huo mkubwa na wa kipekee nchini Tanzania na Afrika, mapema iwezekanavyo, ikiwemo kuanza hatua za ujenzi ndani ya Oktoba 2026.
Amesema hatua hiyo inafuatia uzinduzi wa mtambo mdogo wa uchakataji wa urani uliofanyika mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mavunde ameitaka Mantra kuhakikisha hatua za uendelezaji wa mradi zinaendelea kwa kasi, huku akiuahidi uongozi wa kampuni hiyo kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kila hatua ili kuhakikisha mradi huo unasonga mbele na kuanza uzalishaji ifikapo mwaka 2029.
Katika picha ni Meneja Uendelevu wa Kampuni ya Mantra, Majani Moremi Wambura; kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Vladislav Shulga, na Mjumbe wa Bodi hiyo, Aleksandr Ryabchenko.


0 Maoni