Bandari ya Dar yapania kuhudumia tani milioni 62 kufikia 2031

 

Bandari ya Dar es Salaam imeongeza shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 23.7 mwaka 2023/24 hadi tani milioni 33.7 mwaka 2025/26, huku mipango ya maendeleo ya bandari ikilenga kuongeza uwezo wa kuhudumia tani milioni 62 ifikapo mwaka 2031. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema ongezeko hilo limetokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha kina cha bandari, magati na miundombinu mingine, pamoja na matumizi ya vifaa vya kisasa vinavyoongeza kasi ya upokeaji na uondoshaji wa shehena. 

Gallus amesema ufanisi ulioongezeka umechangia kupungua kwa muda wa meli za makasha kusubiri na kuhudumiwa kutoka zaidi ya siku 30 hadi wastani wa siku tatu, huku ujenzi wa matenki ya mafuta wenye thamani ya shilingi bilioni 678 ukitarajiwa kupunguza zaidi ucheleweshaji wa meli za mafuta na gharama kusubiri zinazowaathiri wafanyabiashara na watumiaji. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema ziara ya waandishi wa habari bandarini imewapa fursa ya kujionea hali halisi ya uendeshaji wa bandari, kufuatia taarifa zilizokuwa zikisambaa kwamba mizigo imekwama na haitoki bandarini. Amesema waandishi wamejionea meli zikiendelea kupakia na kushusha mizigo kwa kasi kwa kutumia vifaa vya kisasa. 

Balile amesema ongezeko la uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam linapaswa kwenda sambamba na upanuzi wa miundombinu ya barabara na reli, ili kuendana na ongezeko la shehena na kupunguza msongamano wa magari, akibainisha kuwa uwezo wa kuhudumia tani milioni 62 utaleta fursa zaidi za biashara, ajira na mapato kwa taifa.




Chapisha Maoni

0 Maoni