WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amesema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuanzisha Wizara maalum yenye dhamana ya kushughulikia masuala ya Mahusiano inaakisi maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha Umoja, Mshikamano na Amani nchini.
“Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa
na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Tanzania
inaendelea kuwa taifa lenye amani, mshikamano na maendeleo kupitia
mazungumzo, maridhiano na ushirikiano wa wadau wote,” amesema
Mhe.
Sangu amesema hayo Juni 28, 2026 katika Ibada maalumu ya kilele cha
harambee iliyofanyika kwenye ushirika wa Amani wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, mjini Singida ambapo
alieleza kuwa Serikali imeendelea kujenga mazingira ya mazungumzo na
ushirikiano kati yake na taasisi za dini ili kuimarisha mshikamano wa
kitaifa.
Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu Mahusiano ni
utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
pamoja na kutimiza wito wa kibiblia wa kuwaleta watu pamoja bila
kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.
Vile vile,
Waziri Sangu amempongeza Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa
kusimamia karibu agenda ya mahusiano nchini, jambo ambalo limewezesha
viongozi wa dini kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao serikalini
kupitia wizara hiyo, hatua ambayo imeongeza ushirikiano na kutatua
changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Aidha, alisema
jukumu la kuwasikiliza wananchi, hususan wanyonge na wenye mahitaji,
ni sehemu ya wajibu wa Serikali na linaendana na mafundisho ya dini
yanayohimiza kuwajali wahitaji na kujenga jamii yenye haki na
mshikamano.
Kwa upande mwengine, Waziri Sangu aliwashukuru
viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake, na
kusema maombi yao yamekuwa nguzo muhimu katika kudumisha amani,
utulivu na maendeleo ya nchini.
Kadhalika, Mhe. Sangu amesema
Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini pamoja
na wadau wengine katika kuimarisha mahusiano ya kijamii na kisiasa,
ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya mazungumzo na vyama vya siasa
kwa lengo la kuimarisha umoja wa Watanzania.

0 Maoni