Kukamilika kwa
mradi wa ujenzi wa daraja la mawe la Kanyunye na ufunguaji wa
barabara yenye urefu wa kilomita 2.6 katika kijiji cha Kanyunye,
wilayani Newala kumeleta suluhisho la kudumu la usafiri na
usafirishaji wa mazao hususani zao la korosho linalozalishwa kwa
wingi katika kijiji hicho.
Akizungumza wakati wa ziara
ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TARURA kupitia mradi wa RISE
programu ya kuondoa vikwazo barabarani (Bottleneck), Meneja wa TARURA
wilaya ya Newala, Mhandisi Silvester Balama amesema waliibua mradi
huo kutokana na changamoto ya mawasiliano ambayo wananchi wa eneo
hilo walikuwa wakikabiliana nayo.
"Wakazi wa kijiji
hiki wengi ni wakulima wa zao la korosho na ghala lao la kihifadhi
korosho zikishavunwa lipo katika kijiji cha Moneka kwa hiyo walikuwa
wanapata shida kusafirisha mazao yao kutoka Kanyunye kwenda Moneka
kwa sababu ya kukosekana kwa kivuko na barabara" ,amesema
Mhandisi Balama.
Ameongeza kuwa ili mazao yao yaweze
kufika katika kijiji cha Moneka ambako ndipo lilipo ghala la
kihifadhia korosho ilikuwa lazima wazunguke upande mwingine katika
vijiji vya wilaya ya Masasi ili waweze kulifikia ghala
hilo.
"Uwepo wa kivuko hiki kumesaidia kutoa mazao
moja kwa moja kutoka kijiji cha Kanyunye kwenda kijiji cha Moneka
ambako kuna ghala lao. Pia kijiji cha Kanyunye hakina shule, shule
yao ya msingi ipo kijiji cha Moneka, watoto walikuwa wanapata shida
sana namna ya kuvuka kwenye mto huu kwa hiyo baada ya ujenzi huu
imekuwa ni ukombozi mkubwa kwao kwa maana sasa watoto wanapita juu na
wanawahi kufika shule".
Bi. Zainabu Mohamedi Seif
mkazi wa kijiji cha Kanyunye amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo
walikuwa wakitembea umbali mrefu kuzifikia huduma za afya hospitali
ambayo ipo mjini Newala lakini sasa hivi wanakodi bodaboda tu kwenda
Newala kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Kwa upande
wake, Bw. Mohamed Seif Hussein maarufu mzee Mchomolo amesema wao kama
wananchi wamefurahishwa na ujenzi wa daraja hilo na kwamba
limewakomboa kwa namna nyingi.
"Hii njia ilikuwa
ni ya kichochoro baada ya kutengeneza barabara na kujengwa hili
daraja sasa hivi imekuwa barabara maarufu ya kupita sio sisi tu bali
hata wenzetu wa kijiji jirani cha Mwanona wameacha kuzunguka huko
sasa hivi wanapita barabara hii kwenda Newala, kabla ya hapo tulikuwa
tunateseka sana" amesema mzee Mchomola.

0 Maoni