TTB kujipanga kunufaika na soko la watalii milioni 13.4 wa Urusi

 

Na. Beda Msimbe (TBN) Petersburg, Urusi

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) inajipanga kumega keki ya utalii inayotengenezwa na Urusi kwa lengo la kulipatia taifa zaidi ya dola za Marekani 500 kwa mwaka.

Zaidi ya wananchi milioni 13.4 wa Urusi hutalii sehemu mbalimbali duniani na kutokana na kuwa watumiaji wazuri wa vipato vyao, Tanzania ikipata angalau asilimia 1 ya watu hao ambacho ni sawa na watu 134,000 ambao wataingiza dola milioni 500.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la Petersburg (SPIEF’26) linaloendelea mjini hapa.

Mafuru alisema katika mikakati hiyo wanataka katika miaka 10 ijayo kufikisha watalii mara mbili ya hao na hivyo kuliingizia pato taifa la dola za Marekani bilioni moja.

Akiwa katika banda la Tanzania katika jukwaa hilo alisema anafurahi kwa Rais Samia kuendelea kuelekeza maono kwa vitendo katika kusaka wawekezaji.


Pia kufungua fursa za Watanzania kwa ziara zinazojumuisha watendaji wakuu wa maeneo muhimu ya taifa kama miundombinu, utalii na madini ili diplomasia ya uchumi iwe na maana kwa taifa.

Mafuru amesema kama nchi wamedhamiria kuhakikisha wanafungua soko la Urusi kwani katika utamaduni wa utalii, wanaongoza duniani na wanaongoza pia kwa matumizi ya kifahari (anasa).

Alisema wamekuwa na mikutano mingi ya utafiti na kubaini watalii hao walikuwa wanashindwa kufika kutokana na umbali lakini kuanza kwa safari za Ndege za ATC za moja kwa moja zitapunguza muda wa kusafiri kwa wananchi hao na kuwa sehemu ya hamasa ya kuja kutembelea Tanzania.

Aidha alisema kwamba wakati umefika kwa wananchi wa tanzania kujifunza Kirusi kwa ajili ya kuvutia watalii ambao hufurahishwa ikiwa wataongozwa kwa lugha ya nyumbani kwao.

Akizungumzia jukwaa na kongamano alisema ziara ya Rais Samia nchini Urusi imekuwa na mafanikio makubwa ambayo yatachangia kukua kwa utalii na pia kusaidia sekta ya uwezekaji na biashara.








Chapisha Maoni

0 Maoni