Ofisi
ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, inapinga na kukanusha vikali taarifa ya uongo
na upotoshaji inayosambaa mitandaoni, ikidai kuwa Dkt. Kikwete
anahusishwa na mradi unaodaiwa kuwa wa uwekezaji unaowaahidi
Watanzania kipato cha uhakika kupitia jukwaa la kifedha linalotumia
teknolojia ya akili mnemba.
Taarifa hiyo inadai kuwa maelfu ya
Watanzania tayari wamenufaika na mradi huo baada ya kuwekeza kiasi
cha shilingi 653,000, huku wakiahidiwa kupata zaidi ya shilingi
9,200,000 kwa mwezi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo.
Ofisi
ya Rais Mstaafu inapenda kuweka wazi kwamba Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete hajawahi kushiriki, kuidhinisha, kutangaza, kuunga
mkono, wala kuhusika kwa namna yoyote ile na mpango huo wa kifedha.
Ofisi yake haijawahi kuruhusu matumizi ya jina, picha, au heshima
yake kuhusishwa na mradi huo unaodaiwa, na haitajihusisha na shughuli
za aina hiyo.
Wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hiyo ya
uongo na kuwa makini dhidi ya miradi ya kitapeli na vitendo haramu
vya aina hiyo. Mtu yeyote atakayekutana na taarifa kama hizo za
upotoshaji anapaswa kuzichukulia kama habari za uongo, kuepuka
kuzisambaza, kujisajili, au kutuma fedha kwa mtu au jukwaa lolote
linalohusishwa nazo.
TAARIFA YA UONGO IPUUZWE.

0 Maoni