Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, amesema vitendo vya kueneza taarifa zinazolenga kuichafua Tanzania vinaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya sasa na ya baadaye ya nchi.
Akizungumza hivi karibuni na wasomi wa Mkoa wa Mbeya, Mwaselela amesema kuna baadhi ya watu wanaofurahia kuona Tanzania ikitajwa vibaya katika majukwaa ya kimataifa bila kuzingatia madhara yanayoweza kuwapata wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema wanaoumia zaidi pale nchi inapopoteza hadhi na sifa yake kimataifa ni wananchi wa kawaida pamoja na watoto ambao mustakabali wao unategemea uwepo wa mazingira mazuri ya uchumi, uwekezaji na maendeleo endelevu.
“Watoto wetu ndiyo wanaobeba gharama kubwa zaidi pale Taifa linapopoteza fursa kutokana na taswira hasi inayojengwa kwa makusudi. Tunapaswa kutambua kuwa maendeleo ya nchi yanahitaji umoja na uzalendo,” amesema.
Mwaselela amesisitiza kuwa ajenda za chuki dhidi ya Tanzania zinapaswa kujibiwa kwa hoja, ukweli na ushahidi badala ya jazba, akibainisha kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda maslahi ya Taifa na kudumisha heshima ya nchi ndani na nje ya mipaka yake.
“Hawa wanaobeba ajenda za chuki wanapaswa kujibiwa kwa hoja na ukweli. Sote tuna wajibu wa kulinda maslahi ya Taifa letu,” amesema.

0 Maoni