Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema anathamini kwa kiwango kikubwa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema umekuwa chanzo cha hamasa na msukumo katika safari yake ya uongozi.
Ameeleza hayo leo Juni 20,2026 wakati akizungumza na wanahabari Ikulu Dar es Salaam, akiambatana na mwenyeji wake Dk. Samia.
Ndaitwah amemshukuru Rais Samia kwa mapokezi mazuri pamoja na fursa ya kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.
Rais Ndaitwah amesema mawasiliano na ushirikiano aliowahi kuwa nao na Rais Samia yameacha alama kubwa kwake na yanaendelea kumwelekeza katika utekelezaji wa majukumu yake ya urais.
“Ninaweza kusema kuwa alinibatiza kwa moto nilipochukua madaraka kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Namibia, na maneno aliyoyasema leo yanaendelea kunipa nguvu na kunihamasisha,” amesema Ndaitwah.
Rais Ndaitwah amesisitiza dhamira ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kindugu kati ya Namibia na Tanzania, akieleza matumaini ya kumpokea Rais Samia nchini Namibia katika siku zijazo ili kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, diplomasia na kubadilishana tamaduni.


0 Maoni