Usemi usemao hakuna marefu
yasiyokuwa na ncha umetimia leo ambapo jumla ya maafisa na Askari 29
kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi
Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya
kimuundo leo tarehe 20 Juni, 2026 katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi
la Uhifadhi kilichopo Mlele mkoani Katavi.
Akifunga mafunzo
hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Meja Jenerali (Mstaafu)
Hamis Semfuko amewataka wahitimu kuzingatia taratibu na sheria na
amri zote za Jeshi la Uhifadhi
“Mmepata mafunzo ya
kubadilika kimuundo kutoka raia kuwa Jeshi, matumaini yangu ni kuwa
kila mmoja wetu hapa mtabadilika na kufanya kazi kwa juhudi na
maarifa katika kusimamia uhifadhi na rasilimali za nchi,” alisema
Meja Jenerali (Mst) Semfuko.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Mhe.
Majid Mwanga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kuwa mfano mwema
wa uzalendo, maadili na ujasiri katika utendaji kazi.
Kwa
upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Abdul-Razaq Badru amewahimiza wahitimu hao kutumia mafunzo
waliyoyapata kuimarisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya
jamii.
Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori
Tanzania (TAWA) Mlage Kabange amesema ushirikiano uliooneshwa kati ya
TAWA na Ngorongoro katika kusimamia mafunzo hayo unaonesha kuimarika
kwa Jeshi la Uhifadhi nchini na ari ya kusimamia rasilimali za
Wanyamapori na Misitu.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo mkuu
wa mafunzo Meja Breyman Rulenguka amesema Jumla wa watumishi 29
wamefaulu na kupata alama za kuridhisha ambapo mwanafunzi mmoja pekee
hakuweza kuhitimu kutokana na sababu za kiafya.
Mafunzo hayo
ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa katika kituo hicho kwa lengo la
kuimarisha Jeshi la Uhifadhi na utendaji kazi wake.




0 Maoni