Serikali
kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ufadhili wa Mfuko wa Mabadiliko
ya Tabianchi ya Kijani (GCF) kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira
la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania
(TAFORI), imefikia hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa
Kujenga Uhimilivu dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika
Mkoa wa Kigoma kwa kuanza uthibitishaji wa matokeo ya tathmini ya
awali ya mradi huo.
Uthibitishaji huo unafanyika kupitia
warsha iliyofanyika katika Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma Juni 26,
2026 ukilenga kuhakiki hali halisi ya kijamii, kiuchumi na
kimazingira katika maeneo ya mradi kabla ya utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za kuimarisha uhimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya
tabianchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo,
Meneja wa Mradi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Onesphory
Kamukuru alisema mradi unatekelezwa katika wilaya za Kasulu, Kibondo
na Kakonko kutokana na maeneo hayo kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na
uharibifu wa mazingira, mmomonyoko wa ardhi na athari nyingine za
mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa mojawapo ya sababu
zilizochangia uharibifu huo ni historia ya maeneo hayo kupokea idadi
kubwa ya wakimbizi, hali iliyosababisha ongezeko la matumizi ya
rasilimali za misitu, ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na
mkaa.
“Mradi huu ni wa wananchi na unatekelezwa katika
maeneo matatu makuu ambayo ni kilimo mseto, usimamizi wa hifadhi za
misitu ya vijiji na za TFS pamoja na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa
na mmomonyoko wa ardhi,” alisema Mhandisi Kamukuru.
Mradi
huo unatekelezwa katika vijiji 22 vya wilaya za Kasulu, Kibondo na
Kakonko, ambavyo vimeathiriwa kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ya
tabianchi na uharibifu wa mazingira, hususan vijiji vilivyo karibu na
maeneo yaliyowahi kuhifadhi wakimbizi.
Katika mradi huu,
TAFORI imepewa jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa za awali
zitakazotumika kama msingi wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji
wa mradi. Aidha, taasisi hiyo inasimamia utekelezaji wa shughuli za
kitaalamu katika maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni Usimamizi
Shirikishi wa Misitu ya Jamii (CBFM), Kilimo Mseto (Agroforestry) na
Upandaji Miti (Afforestation).
Akizungumza kwa niaba ya timu
ya wataalamu wa TAFORI, Mtafiti Mwandamizi na Msimamizi wa Ushauri wa
Kitaalamu wa Mradi, Dkt. Numan Amanzi, alisema matokeo ya tathmini ya
awali yaliyowasilishwa kwa wadau yameridhisha na yanaakisi hali
halisi iliyopo katika vijiji vinavyotekeleza mradi.
“Matokeo
haya yatatumika kama msingi wa kupima mafanikio ya mradi baada ya
kukamilika ili kubaini kwa kiwango gani umechangia kuboresha hali za
kiuchumi, kijamii na kimazingira katika jamii husika,” alisema Dkt.
Amanzi.
Hatua ya uthibitishaji wa matokeo ya tathmini ya awali
ni awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi. Awamu ya kwanza ilihusisha
utambulisho wa mradi kwa mamlaka za Mkoa wa Kigoma na wilaya husika,
huku awamu ya pili ikihusisha uthibitishaji wa vigezo vya uteuzi wa
vijiji, maeneo ya utekelezaji na aina za miti zitakazotumika katika
shughuli za usimamizi shirikishi wa misitu, kilimo mseto na upandaji
miti.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo
wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Maafisa Mazingira,
Maafisa Mkoa, Wilaya, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Wawakilishi
wa vijiji 22 vya wilaya za Kasulu, kibondo na Kakonko.


0 Maoni