WAZIRI
MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda amani,
usalama wa wananchi na rasilimali za Taifa na haitamvumilia mtu
yeyote atakayejihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa
nchi.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 27, 2026)
alipowasalimia wananchi wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, ikiwa ni
sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Waziri Mkuu
amesema Serikali imeendelea kufuatilia taarifa kuhusu watu wanaodaiwa
kupanga au kufadhili vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi na
kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuchukua hatua kwa
mujibu wa sheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo
hivyo.
"Hatutafanya mzaha na mtu wa aina hiyo. Tumepewa
jukumu la kuilinda nchi yetu na watu wake, na hatutafanya mchezo
kwenye jambo hilo."
Amesema Serikali haina mgogoro na
chama chochote cha siasa kwa kuwa vyama hivyo vinatambuliwa na Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali itaendelea kutekeleza wajibu
wake wa kulinda amani, usalama wa Taifa na wananchi wake wakati
wote.
"Hatuna ugomvi na chama chochote cha siasa. Lakini
tuna jambo ambalo ni kipaumbele, usalama wa Tanzania na usalama wa
Watanzania."
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi
kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa
taarifa za vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na kuendelea na
shughuli zao za uzalishaji bila hofu.
Pia amesema Serikali
itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Singida
ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa barabara, reli ya kisasa (SGR),
uwanja wa ndege pamoja na miradi ya maji, afya na elimu kwa lengo la
kuboresha huduma za wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif amesema Serikali
itaendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Singida kuhakikisha
fedha za maendeleo zinaelekezwa katika utekelezaji wa miradi yenye
tija kwa wananchi, huku mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na
halmashauri ikiendelea kuwafikia walengwa kwa wakati.

0 Maoni