Wananchi wametakiwa kutambua
kuwa amani ni mtaji wa kwanza na muhimu katika kuleta maendeleo ya
mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kwani huwezesha uzalishaji,
ibada za dini kufanyika kwa uhuru na kuimarisha mshikamano wa
kijamii.
Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la
Healing Gospel Assemblies of God, John Yakobo, wakati wa ibada ya
uwekaji wakfu wa jengo la kanisa hilo lililopo Bomani, Mjini
Geita.
Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Yakobo amesema ni
muhimu kwa wananchi kutambua na kulinda misingi ya amani kwa kuwa
ndiyo msingi wa mafanikio katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kuhubiri
Injili, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa taifa.
"Amani
ndiyo mtaji wa kwanza wa maendeleo. Bila amani hakuna uzalishaji,
hakuna ustawi wa jamii wala maendeleo ya taifa. Kila mwananchi ana
wajibu wa kuilinda na kuitunza," amesema Askofu Yakobo.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Kanisa la Healing Gospel Assemblies of
God, Godlisten Diah, akinukuu maandiko kutoka Kitabu cha Kumbukumbu
la Torati sura ya nane mstari wa kwanza, aliwahimiza waumini
kuendelea kumtumaini Mungu licha ya changamoto mbalimbali
wanazokutana nazo katika maisha.
"Pamoja na magumu na
majaribu tunayokutana nayo katika maisha, upendo wa Mungu ni mkuu na
wa kudumu. Tunapaswa kuendelea kuwa na imani na kumtegemea Mungu
katika kila hatua," amesema Diah.
Baadhi ya waumini
walioshiriki ibada hiyo walieleza furaha yao kutokana na kukamilika
kwa jengo hilo la kanisa, wakisema litakuwa kitovu muhimu cha kujenga
jamii yenye hofu ya Mungu, maadili mema na mshikamano.
Uwekaji
wakfu wa jengo hilo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha
huduma za kiroho katika Mkoa wa Geita na kuchochea maadili
yanayolenga kujenga taifa lenye umoja, amani na maendeleo endelevu.


0 Maoni