Wananchi
wa kijiji cha Chiuve kata ya Nangomba wilaya ya Nanyumbu mkoani
Mtwara sasa wamepata suluhu ya kudumu ya mawasiliano baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa daraja katika mto Masyalele.
Hayo
yamesemwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Nanyumbu, Mhandisi Dickson
Mkokota wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu
ya barabara katika wilaya hiyo.
Amesema ujenzi wa daraja hilo
lililojengwa katika barabara ya Chiuve-Kalipinde umetekelezwa na
Mkandarasi Central Highway kwa gharama ya shilingi 120,560,360 na
umekamilika kwa asilimia 100.
Mhandisi Mkokota ameongeza kuwa
kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi wa vijiji vya Chiuve na
Kalipinde walikuwa wanatumia kivuko aina ya "drift" ambacho
wakati wa mvua walikuwa wanapata shida kuvuka kutoka upande mmoja
kwenda upande wa pili kwa ajili ya kupata huduma za kijamii na
kiuchumi kama vile hospitali na masoko.
"Manufaa makubwa
yaliyopatikana kwenye mradi huu ni watu wamerahishiwa kuvuka katika
eneo hili la mto", amesema.
Kwa mujibu wa Mhandisi
Mkokota daraja hilo limepewa jina la Somoe Issa kwa sababu kabla ya
ujenzi wa daraja alitokea mama mmoja mjamzito kutoka Kijiji cha
Chiuve kwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya ya Mangaka na kwa
bahati mbaya alipofika katika eneo hilo alikuta maji yamejaa na
kushindwa kuvuka na kujifungua mtoto ambaye amepewa jina la Somoe
Issa hivyo wananchi wa kijiji hicho walipendekeza daraja hilo kuitwa
Somoe Issa.
Kwa upande wake, Bi. Ashura Hamis ambaye ni mama
wa mtoto Somoe Issa mkazi wa kijiji cha Chiuve amemshukuru Rais Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea changamoto hiyo ya muda
mrefu.
"Namshukuru sana mama Samia na serikali yake kwa
hili lililofanyika na kwa wamama wenzangu ambao tumejifungulia
hapa.
Nashukuru kwa kupewa jina la mwanangu daraja hili Somoe
Issa", ameeleza.
Naye, Bw. Rajabu Chakubanga mkazi wa
Mangaka Kilimahewa ambaye ni mkulima amesema ukosefu wa kivuko katika
eneo hilo ilikuwa ni changamoto kubwa kwao hasa wakati wa kusafirisha
mazao yao kutoka mashambani lakini kwa sasa wanashukuru kwani hata
gharama za usafirishaji zimepungua.


0 Maoni