Kaimu Mufti aeleza haja taifa kuzungumza na vijana kujenga maelewano

Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko amesisitiza umuhimu wa taifa zima kutumia fursa mbalimbali kuzungumza na vijana ili kuwalea katika maadili mema na kumcha Mungu, hatua inayosaidia kujenga jamii yenye maadili na maelewano.

Sheikh Ngeruko amesema kuwa vijana ndio nguzo ya kesho ya taifa, hivyo ni muhimu kuwekeza muda, maarifa na malezi bora kwao ili kuhakikisha wanakua katika misingi ya heshima, uadilifu na uwajibikaji katika jamii.

Ameongeza kuwa endapo jamii itawalea vijana katika misingi ya maadili ya kidini na kijamii, itawezekana kupunguza changamoto mbalimbali za kijamii na kujenga kizazi kinachowajibika na chenye mchango chanya kwa taifa.

Sheikh Ngeruko ameyasema hayo wakati akizungumza katika Baraza la Eid al-Adha kitaifa lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, uliopo katika makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kinondoni mkoani Dar es Salaam Mei 27, 2026.
Ametoa wito kwa viongozi wa dini, wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu katika malezi ya vijana, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la pamoja na si la mtu mmoja.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Walid Alhad ametoa wito kwa waumini wa dini ya Kiislamu na Watanzania wote kuendelea kulinda amani ya nchi.

Aidha, Sheikh Walid ametoa wito kwa waumini kutumia sikukuu ya Eid kufanya heri, kusaidiana na kuoneana huruma ili kutafuta radhi za MUNGU.

Chapisha Maoni

0 Maoni