Katibu wa Itikadi, Uenezi na
Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) imeendelea kuleta mageuzi na maendeleo makubwa katika
sekta mbalimbali nchini, huku akiwataka wananchi kutambua tofauti ya
hali ilivyokuwa miaka ya nyuma na ilivyo sasa.
Kihongosi
alitoa kauli hiyo wakati wa hitimisho la ziara ya Mwenezi wa CCM Mkoa
wa Kilimanjaro kabla ya kuelekea Mkoa wa Manyara, akisema ni
upotoshaji kudai kuwa hakuna maendeleo yaliyofanyika nchini kwani
wananchi wanaona na kushuhudia mabadiliko yanayoendelea katika maeneo
mbalimbali.
“Ni makosa kusema hakuna maendeleo nchini.
Wananchi wanaona tofauti ya Tanzania ya jana na ya leo kupitia miradi
na huduma mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na Serikali,”
amesema Kihongosi.
Alieleza kuwa kuongoza taifa kubwa kama
Tanzania si kazi rahisi kutokana na wingi wa wananchi na mahitaji ya
huduma za msingi katika mikoa, wilaya, halmashauri, kata na vijiji,
jambo ambalo linahitaji viongozi wenye maono, uthubutu na uwezo wa
kufanya maamuzi kwa manufaa ya taifa.
Aidha, Kihongosi
alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za
kusimamia maendeleo ya nchi, akisema ameendelea kuelekeza nguvu zake
katika kuwahudumia wananchi licha ya kukabiliwa na ukosoaji kutoka
kwa baadhi ya watu.
“Licha ya changamoto na ukosoaji
anaokutana nao, Rais Samia ameendelea kuweka mbele maslahi ya
wananchi kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na
kuboresha huduma za kijamii,” amesema.
Amesisitiza kuwa CCM
itaendelea kuwaeleza wananchi kuhusu mafanikio ya Serikali na
kuhimiza ushiriki wao katika kulinda na kuendeleza maendeleo
yaliyopatikana nchini.

0 Maoni