WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo
vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho dhidi ya vitendo
vinavyolenga kuvuruga amani ya nchi huku akisisitiza kuwa Serikali
itaendelea kusimamia usalama wa wananchi na mali zao.
“Kuweni
macho na njama za aina hii, shughulikeni na waovu wa aina hii.
Mliweza lile la Kibiti, mliweza lile la Amboni na mambo mengine mengi
mmeweza. Kuweni macho kuhakikisha michezo ya aina hiyo haifanikiwi
huku mkihakikisha usalama wa raia wetu na mali zao unaendelea
kulindwa,” amesema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu amesema hayo
leo Jumamosi, Mei 23, 2026 alipozungumza na wananchi wa Manispaa ya
Iringa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya
Kichangani mkoani Iringa.
Amesema amani ni msingi wa maendeleo
ya Taifa na kwamba Watanzania wanapaswa kuendelea kulinda mshikamano
wa kitaifa na kukataa vitendo vya uchochezi vinavyoweza kusababisha
migawanyiko ya kisiasa, kidini au kijamii.
“Amani ni msingi
wa maendeleo ya taifa letu. Kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha
nchi yetu inaendelea kuwa salama na yenye mshikamano,”
amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema zipo njama mbalimbali
zinazolenga kuwagombanisha Watanzania kupitia siasa, dini na taarifa
za upotoshaji huku akiwataka wananchi kuwa makini na watu
wanaowachochea kufanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa
nchi.
“Tupuuze na wala tusiwe na ushirika na mtu anayekutuma
kuvunja amani wakati yeye hayupo hapo na anajua yeye hataathirika,”
amesema.
Kadhalika, Dkt. Mwigulu amesema baadhi ya matukio
yanayoendelea kujitokeza nchini yakiwemo madai ya watu kujiteka au
kushambuliwa yanapaswa kutazamwa kwa umakini mkubwa kwa kuwa baadhi
yake yanaweza kuwa sehemu ya njama za kuwagawa Watanzania na
kuichonganisha Serikali na wananchi wake.
“Hizi ni ajenda
maalum. Hii ni michezo ambayo inalenga kutengeneza hasira na
kuwafanya watu wachukiane,” amesema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema Serikali imejikita zaidi katika kutatua
changamoto za wananchi na kusukuma maendeleo badala ya kuendelea
kujadili siasa za uchaguzi muda mfupi baada ya uchaguzi mkuu
kumalizika.
“Taifa linapotakiwa kupiga hatua, tujadili namna
ya kutatua kero za wananchi badala ya kutumia muda mwingi kujadili
uchaguzi,” amesema.
Amesema yeye binafsi ameendelea kufanya
ziara mbalimbali za kusikiliza wananchi, kupokea changamoto zao na
kuhakikisha Serikali inazitatua kwa wakati ili wananchi waendelee na
shughuli zao za maendeleo.
“Watu wanahitaji kusikilizwa,
wanahitaji kutatuliwa changamoto zao na wanahitaji maendeleo. Hiyo
ndiyo kazi ambayo Serikali imepewa na wananchi,” amesema.
Aidha,
Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa mshikamano na
uvumilivu wa kidini na kijamii barani Afrika kutokana na misingi
iliyoasisiwa na viongozi waasisi wa Taifa.
“Hii ndiyo nchi
ambayo Mungu ametupatia na Baba wa Taifa ameturithisha. Tukatae
vibaraka wanaotaka kuligawa Taifa letu,” amesema.
Waziri
Mkuu pia amewaomba viongozi wa dini, wazee wa mila, viongozi wa
kisiasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhubiri amani, mshikamano
na uzalendo ili taifa liendelee kuwa salama na lenye umoja.

0 Maoni