Uanzishwaji wa masoko rasmi ya madini pamoja na
matumizi ya mfumo wa bei elekezi mkoani Ruvuma, umetajwa kupunguza
kwa kiasi kikubwa vitendo vya utoroshaji wa madini huku ukiongeza
mapato ya Serikali na kuwanufaisha wachimbaji wadogo.
Mkoa wa
Ruvuma kwa sasa una masoko rasmi ya madini mawili likiwemo Soko la
Dhahabu na Vito la Songea Mjini pamoja na Soko la Dhahabu na Vito
Tunduru, lililozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Septemba 26, 2024.
Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonce Bikulamchi, amesema
mafanikio hayo yametokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali
katika usimamizi wa biashara ya madini kupitia masoko rasmi yenye
uwazi na ushindani wa kibiashara.
Amesema kabla ya kuanzishwa
kwa masoko hayo, baadhi ya wachimbaji walikosa maeneo rasmi ya kuuza
madini yao hali iliyochochea biashara holela na utoroshaji wa madini,
jambo lililoikosesha Serikali mapato na kuwafanya wachimbaji wadogo
kuuza madini yao kwa bei isiyo na tija.
“Kwa sasa wachimbaji
wanapata taarifa sahihi za bei elekezi za madini yao, jambo ambalo
limeongeza uwazi, kuondoa mianya ya udanganyifu na kuongeza imani
katika biashara ya madini,” amesema Mhandisi Bikulamchi.
Ameeleza
kuwa uwepo wa wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi katika masoko hayo
umeongeza ushindani wa bei na kuwawezesha wachimbaji kuuza madini yao
kwa thamani inayostahili.
Aidha, amesema Serikali itaendelea
kuboresha mazingira ya biashara ya madini kwa kuimarisha usimamizi wa
masoko na kutoa elimu kwa wachimbaji ili kuhakikisha sekta hiyo
inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa pamoja na maendeleo ya
wananchi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bikulamchi, hatua hiyo pia
imeongeza ushiriki wa wachimbaji wadogo katika uchumi rasmi na
kusaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini mkoani Ruvuma.


.jpeg)
0 Maoni