Wakala
ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imewahimiza Maafisa
Ununuzi kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi
ili kudhibiti upotevu wa fedha za serikali na kuondoa hoja za ukaguzi
zinazojitokeza mara kwa mara katika utekelezaji wa miradi.
Kauli
hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff
wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wakuu wa
Vitengo vya Ununuzi TARURA kutoka mikoa yote 26 yaliyofanyika mkoani
Morogoro.
Mhandisi Seff alisema mafunzo hayo yamelenga
kuwajengea uwezo wataalamu wa ununuzi kuhusu utekelezaji sahihi wa
sheria ya ununuzi pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto
wanazokutana nazo katika majukumu yao ya kila siku.
Alisema
moja ya changamoto kubwa zinazojitokeza ni kuchaguliwa kwa
wakandarasi wasio na uwezo wa kutekeleza miradi kwa ufanisi pamoja na
udhaifu katika usimamizi wa dhamana mbalimbali za mikataba, hususan
dhamana za malipo ya awali.
"Tumekuwa tukiona
changamoto ya dhamana kupita muda wake hususan dhamana za malipo ya
awali, hali inayosababisha fedha za serikali kupotea na kuwa vigumu
kurejeshwa kutoka kwa wakandarasi waliolipwa", alisema Mhandisi
Seff.
Alieleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalamu
wamepata nafasi ya kujadili kwa kina changamoto hizo na kukumbushwa
wajibu wao wa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa ili
kuhakikisha dosari hizo hazijirudii.
Aidha, alisema
TARURA imejipanga kuhakikisha hoja zinazohusu dhamana zilizopita muda
pamoja na malipo ya awali yasiyorejeshwa hazitaendelea kujitokeza
katika taarifa za ukaguzi.
"Tumekubaliana kwamba
kuanzia sasa hatutegemei tena kuona hoja za ukaguzi zinazohusu
dhamana zilizopita muda au malipo ya awali kutorejeshwa kama
inavyotakiwa kimkataba", alisema.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Ununuzi TARURA, Bw. Venant Majambo
alisema kikao kazi hicho kimelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa
shughuli za ununuzi wa fedha 2025/2026 ambapo zaidi ya asilimia 70 ya
fedha zinazotumika TARURA hupitia katika michakato ya
ununuzi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yataisaidia TARURA
kuingia katika mwaka mpya wa fedha 2026/2027 ikiwa na wataalamu wenye
uelewa mpana wa sheria na taratibu za ununuzi, hatua itakayosaidia
kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za
umma.
Bw. Majambo alisema TARURA inalenga kupunguza
mapungufu yanayobainishwa katika taarifa za ukaguzi kutoka kwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), PPRA pamoja na
wakaguzi wa ndani kupitia usimamizi madhubuti wa shughuli za ununuzi.


0 Maoni