Mawakili tuwe watetezi wa serikali

 

Mawakili wa Serikali wametakiwa kuendelea kuwa watetezi wa Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake.

Hayo yameelezwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali uliofanyika jijini Arusha.

“Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mtambue mna jukumu la kuendelea kuitetea Ofisi na Serikali mahakamani katika uendeshaji wa mashauri ili tulinde maslahi ya taifa letu,” amesema Dkt. Possi.

Pia, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na upendo ndani ya taasisi kwa kuwa hii ni afya kwa taasisi na nchi yetu na hili liwe mpaka chini kwa watumishi wote.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo aliwapongeza watumishi wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano wa pamoja na mwenendo huu unaendelea kuijengea heshima Ofisi na ina akisi ukomavu wa Ofisi.

“Kila kiungo ni muhimu, mchango wa kila mtumishi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa tunafikia malengo yaliyowekwa,” amesisitiza Bi. Mtulo.

Bi. Mtulo amewaeleza watumishi hao kuwa Serikali ina matarajio makubwa kutoka kwao. Hivyo, kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, maadili ya utumishi wa umma na viwango vya taaluma tulivyojiwekea ili tuwe na utamaduni wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Mkutano huo hufanyika mara moja kwa mwaka ili kuwakutanisha watumishi wote kwa lengo la kujadiliana kuhusu mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji majukumu, changamoto, kupata mafunzo mbalimbali ya kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa mtumishi mmoja mmoja ili kujenga Ofisi yenye mshikamano na mazingira mazuri ya kazi.

Mkutano huo umefanyika kwa siku mbili tarehe 21 na 22 Mei, 2026 na kuwakutanisha watumishi wote wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zilizopo kwenye mikoa 18 Tanzania Bara.



Chapisha Maoni

0 Maoni