Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera (Mb) amefungua mafunzo ya
Mawakili wa Serikali yanayohusu Mawakili wa Serikali wa kutoka
Wizara, Idara, taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za
mitaa wa Tanzania Bara na Zanzibar ambayo yanafanyika jijini Arusha.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na
yanafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Mei, 2026.
Mafunzo hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, ”Kulitumikia Taifa
katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ili kulinda
maslahi mapana ya taifa kwa ajili ya kesho.”
Mhe. Dkt.
Homera amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria
inaamini kwamba hakuna maendeleo endelevu bila mfumo imara wa
kisheria na wala hakuna uchumi shindani bila utawala bora. Wizara
inaamini kuwa Sekta ya sheria siyo tu ni muhimili wa utawala bora
bali ni miundombinu isiyoonekana inayoshikilia misingi ya kiuchumi
ya nchi.
Ameongeza kuwa Dira 2050 imeweka misingi yake katika
Sekta ya Sheria ambayo ni utawala, amani, usalama na utulivu. Kwa
kuzingatia kuwa katika kipindi hiki cha ushindani wa kimataifa na
kiuchumi, pamoja na mambo mengine taifa linahitaji watu wake walio
imara katika kusimamia sheria zitakazoleta amani, utulivu, maendeleo
ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla. ”Hivyo, ni lazima kwa
Mawakili wa Serikali ambao ndio watekelezaji namba moja wa Dira 2050
kuwa imara katika kushauri, kutetea na kulinda rasilimali na maslahi
ya Taifa hili. Niipongeze Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa
kuandaa mafunzo haya kwa Mawakili ili kuhakikisha kuwa Sekta ya
Sheria inashikilia misingi ya kiuchumi ya nchi,” amefafanua Mhe.
Dkt. Homera.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amesema
kuwa lengo la Ofisi kutoa mafunzo hayo ni kuendelea kuwanoa Mawakili
ili kuwa askari wa kalamu katika kulinda maslahi ya taifa tangu hatua
ya awali ya uandaaji wa mikataba, usimamizi wa mikataba na usuluhishi
wa migogoro kabla na baada ya kuwasilisha shauri katika Mahakama na
Mabaraza.
Dkt. Possi amesema kuwa katika kipindi cha mwezi
Julai, 2025 hadi Machi, 2026, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
imepata mafanikio mbali mbali ikiwemo uendeshaji wa mashauri 641 ya
madai yaliyohitimishwa na kushinda mashauri 565 ambayo ni sawa na
asilimia 88.1 ya mashauri yaliyomalizika na kuokoa jumla ya shilingi
bilioni 316.28 ambazo Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri
hayo.
Pia, Ofisi imehitimisha mashauri 18 ya usuluhishi na
kuiwezesha Serikali kuokoa shilingi bilioni 6.8 na dola za Marekani
milioni 418.17 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.09 ambazo
Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo. ”Hivyo, jumla
ya shilingi trilioni 1.35 zimeokolewa katika uendeshaji wa mashauri
ya madai na usuluhishi katika kipindi tajwa hapo juu ambapo Serikali
ingeshindwa tungelipa pesa hizo,” amefafanua Dkt. Possi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali
wasome na kuzingatia utekelezaji wa Dira ya 2050 ili kuhakikisha nchi
inakuwa na amani, utulivu na misingi thabiti ya utawala wa sheria na
watumie fursa ya mafunzo haya kujadiliana namna ya kutetea na kulinda
maslahi ya taifa nje ya mahakama.
Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali, Bi. Alice E. Mtulo amesema kuwa Mawakili hao watapatiwa
mafunzo na wataalam wabobezi wa sheria za usafiri wa anga, uandishi
wa sheria, sheria za kodi katika sekta ya gesi na madini ; usimamizi
wa mikataba na mamlaka ya usikilizaji wa rufaa za zabuni ; pamoja na
uendeshaji na usikilizaji wa mashauri ya madai na usuluhishi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na Mawakili wa Serikali wakati wa mafunzo kwa Mawakili hao yaliyofanyika Jijini Arusha.




0 Maoni