Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Masanja Kadogosa, imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji yanayoendelea kuihusisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na sekta ya uchukuzi kwa ujumla.
Akizungumza baada ya
ziara ya kamati hiyo bandarini hapo Mei 23, 2026, Kadogosa amesema
maboresho yanayoendelea yameongeza ufanisi na kutoa nafasi kwa sekta
binafsi kushiriki moja kwa moja katika kuongeza tija ya shughuli za
bandari.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame
Mbarawa, amesema Serikali imeweka msukumo mkubwa wa ushirikiano na
sekta binafsi katika miundombinu ya bandari, reli na usafirishaji ili
kuongeza ufanisi na ushindani wa kiuchumi. “Ufanisi wa Bandari ya
Dar es Salaam umeongezeka kutoka wastani wa kushughulikia makontena
61,000 hadi zaidi ya 110,000 kwa mwezi,” amesema Prof.
Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea na
mipango ya upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati 11 pamoja na
kuimarisha Bandari ya Bagamoyo, huku akisisitiza kuwa ushirikiano na
sekta binafsi ndio nguzo kuu ya mafanikio hayo.
Amesema pia maboresho ya miundombinu ya reli ikiwemo TAZARA yanalenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kutoka nchi jirani, hatua itakayoiweka Tanzania katika ushindani mkubwa wa kikanda dhidi ya bandari za Mombasa na Durban.

0 Maoni