Kidoti Foundation yajipanga kuimarisha fursa kwa vijana kupitia michezo

 

Mwanzilishi wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo, amesema taasisi hiyo inalenga kupanua mtandao wa ushirikiano na wadau wenye ushawishi mkubwa kimataifa katika sekta ya michezo, uongozi na maendeleo ya vijana.

Jokate ameyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo maalumu na kiongozi wa michezo wa NBA na mwanzilishi wa Giants of Africa, Masai Ujiri, jijini Kigali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Kidoti Foundation.

Amesema safari hiyo inalenga kujenga mahusiano yatakayosaidia kufungua fursa zaidi kwa vijana wa Kitanzania kupitia michezo, uongozi na ushauri nasaha. “Tumekuja Kigali kwa ajili ya mazungumzo na Masai kama sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa taasisi yetu, lakini pia kujenga ushirikiano utakaowezesha vijana wetu kunufaika zaidi,” amesema Jokate.

Kupitia taasisi ya Giants of Africa, Masai Ujiri ameendelea na kampeni ya kujenga viwanja 100 vya mpira wa kikapu barani Afrika, ambapo nusu tayari vimekamilika katika nchi mbalimbali. 

Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo baada ya kujengwa kwa kiwanja katika Shule ya Sekondari Minaki, Kisarawe, hatua inayolenga kukuza vipaji na kutumia michezo kama chombo cha maendeleo ya jamii.


Chapisha Maoni

0 Maoni