Mwanadiplomasia na Mratibu wa Makongamano ya Vijana, Ndugu Omary Abdul Punzi, ametoa onyo kwa vijana nchini kuacha kufuata mikumbo isiyo na tija na badala yake waithamini nchi yao kwa kutanguliza uzalendo mbele.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Vuka Blog, Punzi
amesisitiza kuwa amani ya nchi haitofautiani na utulivu wa kisiasa,
bali inategemea kwa kiasi kikubwa jinsi vijana wanavyoheshimu
utamaduni wao na kushirikiana kikamilifu na mihimili nane muhimu
inayolinda na kulea taifa.
Amewasihi vijana kuwa makini na
ushawishi hasi wa utandawazi na makundi yasiyo na maadili
yanayotishia mustakabali wa nchi.
Akionyesha masikitiko yake,
Punzi amekumbusha kuwa Tanzania ni urithi wa thamani tulioachiwa na
waasisi wetu, hivyo hakuna nchi nyingine mbadala ikiwa vijana
wataharibu hii iliyopo.
Alibainisha kuwa miongozo na desturi
nzuri zilizowekwa na wazee wa kimila tangu zamani hazikuwa za
kizamani, bali zililenga kulinda utu na heshima ya jamii.
Alionya
kuwa sasa vijana wanatupa dhahabu yao kwa sababu tu inaonekana ya
kienyeji na kuokota shaba ya kigeni kwa kuwa inang’aa, jambo
linalohitaji mabadiliko ili mila na desturi zilizokubalika zisafishwe
na kuendelezwa badala ya kufutwa kabisa.
Katika uchambuzi
wake, Punzi alifafanua jinsi mihimili nane ya amani na malezi
inavyopaswa kuwa dira kwa kijana mzalendo. Mhimili wa kwanza ni shule
ambayo ndiyo msingi wa maarifa, nidhamu na malezi ya awali ya kiakili
yanayomfanya kijana kuwa raia mwema.
Hii inaenda sambamba na
Jeshi la Polisi ambalo ni chombo cha usalama wa raia na mali zao
kinachotegemea ushirikiano wa karibu na vijana kupitia ulinzi
shirikishi. Vivyo hivyo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linatajwa kama
jukwaa la kuwajenga vijana katika ukakamavu na uzalendo, huku Jeshi
la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) likiwa ngome kuu ya ulinzi wa
mipaka ya nchi na alama ya mamlaka ya taifa.
Mihimili mingine
inayokamilisha ngome hii ya malezi na ulinzi inajumuisha Idara ya
Usalama wa Taifa, chama cha Skauti, taasisi za kidini, pamoja na mila
na desturi nzuri ambazo ndizo msingi wa utambulisho wa Mwafrika
unaosisitiza heshima, mshikamano na utatuzi wa migogoro kwa njia ya
mazungumzo badala ya vurugu.
Punzi amewataka vijana
kutokubali kuwa bendera inayofuata upepo wa mambo yanayoonekana
maarufu kwenye mitandao ya kigeni, kwani kufanya hivyo ni kupoteza
dira. Alizitaka taasisi zote za elimu, dini na vikosi vya usalama
kushirikiana kwa karibu ili kuwatengenezea vijana mazingira wezeshi
yatakayowafanya kuwa walinzi namba moja wa amani na maendeleo ya
Tanzania.

0 Maoni