Mkoa wa
Ruvuma umeendelea kujizolea umaarufu katika sekta ya madini baada ya
makaa ya mawe yanayochimbwa katika wilaya za Mbinga, Songea na Nyasa
kufungua masoko katika nchi mbalimbali za Afrika na Asia, huku zaidi
ya tani milioni 3.6 zikizalishwa mwaka 2024/2025 na kuchochea ajira,
biashara na matumizi ya nishati safi.
Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema shughuli za
utafiti, uchimbaji na uchakataji wa makaa ya mawe zinazofanywa na
makampuni pamoja na wadau mbalimbali zimekuwa na mchango mkubwa
katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Amesema
makaa hayo yenye ubora wa hali ya juu yanatumika katika viwanda vya
saruji, usafishaji wa vyuma na shughuli nyingine za viwandani, huku
sehemu ya uzalishaji ikipelekwa katika masoko ya Kenya, Uganda,
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Migodi ya
makaa ya mawe ya Ruvuma imeendelea kuvutia wawekezaji kutokana na
ubora wa madini hayo, hali iliyosaidia kufungua masoko mapya katika
baadhi ya nchi za Asia na Ulaya,” amesema Mhandisi
Bikulamchi.
Ameeleza kuwa ukuaji wa sekta hiyo umechangiwa na
kuongezeka kwa uwekezaji pamoja na mahitaji ya nishati duniani tangu
mwaka 2019/2020, jambo lililoongeza mchango wa sekta ya madini katika
mapato ya Serikali na maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma.
Katika
hatua nyingine, wadau wa makaa ya mawe mkoani humo wameendelea kuunga
mkono agenda ya matumizi ya nishati safi kupitia uzalishaji wa mkaa
mbadala unaotokana na makaa ya mawe, wakiwemo Mgodi wa Jitegemee
uliopo Wilaya ya Mbinga na Kampuni ya Suzlon ya Wilaya ya
Songea.
Migodi hiyo imeendelea kuzalisha mkaa wa nishati safi
unaotajwa kusaidia kupunguza matumizi ya mkaa wa kawaida unaotokana
na ukataji miti, hatua inayochangia uhifadhi wa mazingira na
kupunguza uharibifu wa misitu.
Msimamizi wa Mauzo na
Uendeshaji wa Mgodi wa Jitegemee, Mark Tarimo amesema kampuni hiyo
imetoa zaidi ya ajira 500 kupitia nafasi za kudumu na mikataba ya
mwaka mmoja, huku bidhaa zake zikisafirishwa katika nchi za Afrika
Mashariki na Falme za Kiarabu (UAE).
Tarimo amesema kampuni
hiyo pia imetekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa
shule katika Kijiji cha Ruanda, zahanati katika Kijiji cha Luhagara
pamoja na usambazaji wa majiko ya nishati safi kwa wananchi.
Naye
Mkurugenzi wa Mgodi wa Suzlon, Jigar Chandarana amesema mkaa wa
nishati safi unaozalishwa na kampuni hiyo ni mbadala wa mkaa wa
kawaida kwa kuwa hudumu kwa muda mrefu, ni nafuu kwa matumizi ya
nyumbani na husaidia kulinda mazingira dhidi ya uharibifu wa
misitu.
Aidha, Mhandisi Bikulamchi amewataka wawekezaji wa
ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini
mkoani Ruvuma, huku akiwahimiza vijana kushiriki katika shughuli za
uchimbaji, usafirishaji na utoaji wa huduma zinazohusiana na sekta
hiyo.


0 Maoni