Mwanasayansi
bingwa kutoka Tanzania, Sospeter Mwijarubi Muhongo, amechaguliwa kuwa
mjumbe wa Baraza la Uongozi la Wasomi wa Sayansi Afrika (AAS) kwa
kipindi cha mwaka 2026 hadi 2029.
Katika uchaguzi wa
kielektroniki uliofanyika hivi karibuni, Profesa Muhongo alipata kura
168 za ndiyo, kura mbili za hapana na kura 15 za kutokuegemea upande
wowote, huku asilimia 74.60 ya wajumbe wenye sifa wakishiriki kupiga
kura.
Kwa mujibu wa wasifu wake mfupi, Profesa Muhongo ni
msomi mashuhuri wa kiwango cha kimataifa katika sayansi ya dunia na
mwanajiolojia aliyesajiliwa barani Ulaya.
Ana shahada ya
uzamivu ya Dr.rer.nat. kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin
nchini Ujerumani.
Mbali na kuwa Waziri wa zamani wa Nishati na
Madini wa Tanzania, Profesa Muhongo pia aliwahi kuwa Rais wa Jamii ya
Wanajiolojia Afrika na ni mwanachama mwandamizi wa AAS.
Aidha,
ametunukiwa hadhi ya Honorary Fellow na Geological Society of London
pamoja na Geological Society of America. Pia ni Honorary Research
Fellow wa Chinese Academy of Geological Sciences.
Profesa
Muhongo pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Kanda ya Afrika wa
Umoja wa Baraza la Kimataifa la Wanasayansi (ICSU).

0 Maoni