Mbeto awasihi Wanasiasa na Wasomi kulinda amani

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, kimewataka viongozi wastaafu, wasomi, wachambuzi na wanasiasa kulinda umoja na amani ya nchi.

Mbeto amesema gharama ya kujenga Taifa ni kubwa kuliko hasara ya kulibomoa, akisisitiza umuhimu wa viongozi na wadau mbalimbali kuwa waandishi na wasemaji wa heri badala ya kupandikiza chuki na hasama katika jamii.

Aidha, amekemea tabia iliyoibuka hivi karibuni ya baadhi ya viongozi wastaafu na wanataaluma wanaotoa kauli kali na za kuogofya bila kupima athari zake kwa jamii. Amesema maneno yasiyochujwa yanaweza kuleta madhara makubwa na kusababisha taharuki isiyo ya lazima.

“Ghasia na machafuko yakizuka hayana macho; huwadhuru wote matajiri, maskini, viongozi na raia wasio na hatia,” amesema Mbeto.

Katika hatua nyingine, Mbeto amewasihi wadau hao kutumia njia za kiungwana na mazungumzo katika kutatua changamoto za kisiasa na kijamii badala ya kutafuta umaarufu kupitia kauli za uchochezi.

Pia, ameonya kuwa siasa za kuhubiri chuki na shari zimechangia kubomoka kwa baadhi ya mataifa barani Afrika kutokana na vita na umwagaji damu, huku akisisitiza kuwa njia halali ya kupata madaraka ni kupitia demokrasia ya uchaguzi na si kwa vurugu.

Chapisha Maoni

0 Maoni