Vyama
12 vya siasa nchini vimejitokeza kwa pamoja kupongeza ripoti ya Tume
ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, vikisema imegusa kwa kina
changamoto zilizojitokeza na kutoa mapendekezo yenye mwelekeo wa
kulinda amani na mshikamano wa kitaifa. Aidha, vyama hivyo vimetaka
kuharakishwa kwa mchakato wa maridhiano pamoja na kupatikana kwa
Katiba mpya, kama ilivyopendekezwa na tume hiyo.
Akizungumza
leo Aprili 26, 2026 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa
habari, wawakilishi wa vyama hivyo walisema pendekezo la kuanza
mchakato wa Katiba mpya kabla ya mwaka 2028 linapaswa kupewa uzito wa
kipekee. Walisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa suluhu ya kudumu
kwa changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinazoikabili nchi kwa
sasa.
Vyama vilivyoshiriki katika tamko hilo la pamoja ni DP,
NRA, NLD, AAFP, ADA-TADEA, Demokrasia Makini, UPDP, UDP, SAU, UMD,
TLP na CCK, vikionyesha mshikamano wa nadra katika masuala ya msingi
ya kitaifa. Kauli yao ya pamoja imeelezwa kuwa ishara ya utayari wa
kushirikiana kwa lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora
nchini.
Katika tamko hilo, vyama hivyo vimesisitiza kuwa viko
tayari kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mapendekezo
yote yaliyotolewa na tume, wakieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu
katika kudumisha amani, utulivu na kuondoa migogoro ya kisiasa
inayoweza kujitokeza siku zijazo.
Akizungumza kwa niaba ya
vyama hivyo, Hassan Doyo, aliyekuwa mgombea urais kupitia NLD katika
uchaguzi mkuu wa 2025, alisema kupatikana kwa Katiba mpya hakutaishia
kutatua changamoto za kisiasa pekee, bali pia kutasaidia kulijenga
upya Taifa na kurejesha imani miongoni mwa wananchi. “Kupitia
maridhiano na Katiba mpya, nchi itaendelea kuwa na amani na utulivu
wa kudumu,” alisisitiza Doyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
jukwaa hilo, Abdul Muya, alimpongeza mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed
Othman Chande, kwa kazi kubwa iliyofanywa, akieleza kuwa ripoti hiyo
imeweka msingi imara wa majadiliano ya kitaifa. Pia alitoa wito wa
kuitishwa kwa Baraza la Vyama vya Siasa ili kujadili kwa kina
mapendekezo yote yaliyomo kwenye ripoti hiyo na kuweka mkakati wa
utekelezaji wake.
Muya aliongeza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya
dola kuchukua hatua stahiki dhidi ya vichocheo vilivyotajwa kwenye
ripoti hiyo kama sababu ya ghasia za Oktoba 2025, ili kuzuia matukio
kama hayo kujirudia. Alisisitiza kuwa uwajibikaji ni sehemu muhimu ya
mchakato wa maridhiano ya kweli.
Wakati Rais Samia Suluhu
Hassan, alipokuwa akipokea ripoti hiyo, alieleza dhamira ya Serikali
yake kuhakikisha upatikanaji wa Katiba mpya katika kipindi chake cha
pili cha uongozi. Pia alitangaza kuundwa kwa Tume ya Maridhiano
katika siku za karibuni, itakayokuwa na jukumu la kuratibu na
kusimamia mchakato mzima wa maridhiano nchini.
#UmojaWetuNdiyoNguvuYetu
#turidhiane

0 Maoni